Mataifa ya magharibi na yale ya kiarabu jana yameahidi mchango wa dola bilioni 1.8 kuisaidia Sudan inayoandamwa na hali mbaya uchumi, mwaka mmoja tangu vuguvugu la demokrasia lilipoung´oa utawala wa muda mrefu wa rais Omar al-Bashir.
Ahadi hiyo kutoka zaidi ya mataifa 40 ikiwemo msaada wa nyongeza wa dola milioni 400 kutoka benki ya dunia, imetolewa wakati wa mkutano uliotishwa na Ujerumani kwa lengo la kuisaidia serikali ya mpito nchini Sudan baada ya miongo kadhaa ya vikwazo vya kiuchumi na kutengwa kimataifa chini ya utawala wa al-Bashir.
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas aliuambia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video kuwa msaada uliotolewa ni hatua ya kwanza ya kuisaidia Sudan na kwamba kutakwua na mkutano mwingine wa wafadhili mapema mwaka unaokuja.
Hata hivyo kiwango kilichotolewa na mkutano huo ni kidogo ikilinganishwa na ombi la dola bilioni 8 lililotolewa na serikali ya Sudan ili kunusuru uchumi wa taifa hilo unaoandamwa na ukosefu wa ajira na athari za janga la virusi vya corona.
