Wakazi wa Kidomole walilia mawasiliano ya simu



Na Omary Mngindo, Kidomole.

WAKAZI wa Kijiji cha Kidomole Kata ya Fukayosi wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamewaomba wamiliki wa kampuni za simu kuboresha mawasiliano kwenye maeneo yao.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari kijijini hapo kwaniaba ya wenzao, Emmanuel Pantaleo na Shakila Hamisi walisema kuwa wanakabiliwa na adha ya mawasiliano, huku Pentaleo akieleza kuwa yeye anajihusisha na huduma za pesa kupitia nitandao mbalimbali, hali inayompatia changamoto kubwa

Pentaleo alisema kuwa mara kadhaa anapompatia mteja huduma ya kuweka au kupokea pesa kupitia mitandao hiyo analazimika kutoka ndani ya duka lake kuelekea kwenye barabara ya Bagamoyo Kiwangwa Msata ili apate mawasiliano ya kutuma au kutoa pesa.

"Kama ulivyoshuhudia hata wewe mwenyewe Mwandishi ulipotaka kutoa pesa, imekuchukua dakika kadhaa kufanikisha zoezi hilo sasa changamoto hii imekuwa kubwa kwa miaka mingi huku kukiwa hakuna dalili za kuondokana na adha hii," alisema Pentaleo.

Kwa upande wake Shakila alisema kwamba yeye anapohitaji kupiga simu analazimika kutoka nyumbani kwake kuja maeneo ya barabarani ili kuweza kupata mawasiliano ya kupiga simu, na kwamba wakazi hao simu zao huziweka juu ya ukuta wa nyumba, inapoita wanaitafuta barabara ili wazungumze.

"Leo tunashukuru kutembelewa na chombo cha habari kijijini kwetu, tunaimani kwamba kilio hiki kitawafikia viongozi husika, hatimae kiweze kupata ufumbuzi, suala hili limekuwa kero kubwa sana kwa wana-Kidomole," alisema Shakila.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mrisho Some alisema kwamba wakazi kijijini hapo sana kiu ya miaka mingi kuhusiana na adha ya mawasiliano, hivyo amewaomba wamiliki wafike waangalie namna gani wanavyoweza kupunguza kana si kumaliza adha hiyo.

"Kijiji chetu pekee kina wakazi 796 ambapo kati yao wanamiliki simu hivyo wanaathirika na upatikanaji wa mawasiliano, tunawaomba wamiliki au Mamlaka ya Mawasiliano TCRA wasikilize kilio hiki," alimalizia Some.