Waziri wa Elimu Zanzibar afanya ziara katika shule Unguja


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma amefanya ziara katika Skuli za Unguja kwa ajili ya kukagua hali ya Mitihani ya Taifa ya kidato cha sita ilivyoanza.

Katika ziara hiyo Riziki amepata nafasi ya kuzungumza na Wanafunzi  ambapo amewataka Wanafunzi watahiniwa, kuepukana na udanganyifu wa aina yoyote wanapokuwa katika mitihani yao.

Alisema kujiamini wakati wa kufanya Mitihani ndio njia pekee itakayowasaidia kujibu vyema Mitihani yao na kuweza kupata ufaulu wa daraja la juu.

Riziki aliwataka  Wanafunzi kuhakikisha  wanasoma maelezo ya Mtihani unavyoelekeza  vizuri kabla ya kujibu maswali ili waweze kujibu majibu ya uhakika kwa kile walichoulizwa.

Aidha Waziri  alisema ni lengo la Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu kuondosha  kabisa  zero na kupunguza alama za daraja la nne ili  Taifa lizalishe  wataalam mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mwalimu msimamizi wa Mitihani katika Skuli ya Dk Ali Mohamed Shein iliopo Mwembeladu, Meja Mstaafu Zagu Haji Zagu alimpongeza Waziri wa Elimu kwa utaratibu aliojiwekea kuhakikisha anapita katika  Skuli kuhamasisha Wanafunzi kufanya vizuri katika Mitihani yao,hali hiyo itawapa moya Wanafunzi na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Nae mwanafunzi Amne  Pembe Ali kwa niaba ya Wanafunzi wenziwe alimuhakikishia Mhe Riziki kuwa pamoja na  kupitia  wakati mgumu  wa kufungwa Skuli kutokana na maradhi ya covid 19 lakini  watafanya vizuri katika Mitihani yao na kufaulu daraja la kwanza.

Katika ziara hiyo Waziri alipata nafasi ya kukagua katika Skuli ya Lumumba, Jang'ombe, Haile sselassie, Hamamni na Kiponda, ambapo jumla ya Wanafunzi  2686 wa kidato cha sita kwa Skuli za Zanzibar wameanza Mitihani yao leo.