Afikishwa Mahakamani kwa tuhuma za kubaka na kumpa mimba mwanafunzi


Na Amiri Kilagalila, Njombe
Julai 14,2020 mshtakiwa Luka Nelikon Mahenge (18) mkazi wa kijiji cha Isapulano wilaya ya Makete mkoa wa Njombe amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Makete akituhumiwa kwa makosa mawili ya kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya Sekondari Iwawa (17).

Imeelezwa mnamo Julai 10,2020 majira ya saa 9 alasiri katika kijiji cha  Iwawa kilichopo wilaya ya Makete Mkoani Njombe  bila halali mshtakiwa alimbaka mwanafunzi Huyo jina limehifadhiwa  mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Sekondari Iwawa kinyume na  kifungu namba 130 kifungu kidogo 1 na 2 [e]  na kifungu cha 131 kifungu kidogo 1 vyote vifungu vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Pia mshtakiwa huyo amesomewa shitaka la Pili ambapo bila halali anashtakiwa  kumpa   mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari Iwawa mwenye umri wa miaka 17 (jina limehifadhiwa) kinyume na kifungu namba 60 [A]  kifungu kidogo cha 3 cha sheria ya elimu  kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria ya bunge namba 2 ya mwaka 2016.

Aidha mshtakiwa huyo amekana makosa yote mawili  na shauri hilo limeahirishwa na hakimu mfawidhi wa wilaya ya makete Mh John Mpitanjia  chini ya mwendesha mashtaka Benstard Mwoshe kwa ajili ya usomaji wa hoja za awali mpaka Julai 21 2020.

Hata hivyo mshtakiwa amepelekwa mahabusu baada ya Kushindwa Kukidhi masharti ya Dhamana ya  kudhaminiwa kwa shilingi milioni 5.

Wakati huo huo mahakama ya wilaya ya makete imeendelea kusikiliza shauri namba 32 la jamuhuri dhidi ya Felix Zainab Sanga anayeshtakiwa kwa makosa mawili  La Kubaka na Kumpa Mimba Mwanafunzi wa Darsa la Saba katika shule ya msingi Igolwa (17) jina Linahifadhiwa ambapo shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 20 Julai 2020 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana