Chadema yampitisha Magreth Kyai Kugombea Ubunge Missenyi Kagera

Na Clavery Christian Missenyi Kagera,
Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA wilayani missenyi mkoani Kagera kimempitia bi Magreth Kyai kugombea ubunge katika jimbo la Nkenge wilayani humo.

Akitangaza matokeo katika kikao kilicholenga kuwapigia kura za maoni wagombea,katibu wa chama hicho wilayani Missenyi bwana Ruchius Joseph amesema kuwa bi Magreth amepitishwa baada ya mgombea mwenza aliyetajwa kwa jina la Hilda Luhikula kujiondoa katika mchakato ili kumpisha mwenzake aweze kuwatumikia wananchi.

Bwana Ruchius ameongeza kuwa mgombea huyo kwa sasa anasubiri kuidhinishwa katika vikao ngazi ya mkoa ili aweze kuanza rasmi kampeni pindi pazia la kampeni litakapofunguliwa.

Naye mgombea ubunge aliyepitishwa bi Magreth Kyai amesema kuwa ameamua kugombea nafasi hiyo ili aweze kujenga hoja zitakazosaidia kuimarisha kilimo cha kahawa na kuwakomboa kiuchumi wananchi wa mkoa wa Kagera.

Aidha bi Magreth ameongeza kuwa anakusudia kuhakikisha anafungua milango na fursa za kiuchumi kwa jimbo la Nkenge kwa kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika kilimo na ufugaji wilayani humo.