Ali Khatibu Achukua fomu ya kugombea Urais,Ada-Tadea



Na Thabit Madai,Zanzibar.

MWANACHAMA wa chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib amejitokeza kuchukua fomu ya kutia nia ya kugombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo katika makao Makuu ya chamahicho Kwamchina, alisema ikiwa chama kitampa ridhaa ya kugombea nafasi hiyo basi ataendelea kuwa mumini wa kulinda Mapinduzi Matukufu ya m waka 1964 na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliosisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Juma ambae ni Waziri asiyekuwa na Wizara maalum alisema endapo wananchi watamchagua na kupata ridhaa basi kipaumbele chake ni kutekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya utawala wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.


Akiitaja miradi hiyo alisema ni pamoja na bandari ya Mpiga duri, bandari ya mafuta na gesi Mangapwani, Hospitali ya Binguni na kituo kikubwa cha Afya na ujenzi wa nyumba za maendeleo kwahani. 
"Nikiwa kama waziri nisiekuwa na qwizara maalum nafahamu juhudi za Dk. Shein, serikali na wapi tumefikia katika miradi hii hivyo naahidi nikiwa kama msaidizi wake basi nitahakikisha natekeleza kwanza miradi hii mikubwa ya maendeleo,"alisema.

Aidha alisema eneo jengine atakalolifanyia kazi ni kuendeleza uchumi wa bluu kwa kuhakikisha bei ya mwani inaendelea kuongezeka kwani tayari serikali imeshaanza kujenga misingi imara na mikakati kwa kujenga kiwanda cha kusarifu mwani Chamanangwe kisiwani Pemba.

Alisema ni jukumu lake atakapopata ridhaa kuendeleza kazi zote zilizoanzishwa na serikali chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya saba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

"Serikali ya awamu ya saba imefufua kampuni ya ZAFICO na nahidi kama nitapata ridhaa ya chama na wananchi basi nitaendeleza kazi hizi zilizoacha na Dk. Ali Mohamed Shein kwa msingi ya kuwaletea maendeleo zaidi wananchi wa Zanzibar na kupata ajira na maisha mazuri," alisma.

Alisema akimaliza miradi hiyo mikubwa ataangalia sera ya chama chake kwa kutoa posho maalum kwa wazazi wote wanaokwenda kujifungua kwa muda wa miaka miwili na kuendeleza  pencheni ya wazee wanaotimiza umri wa miaka 70 iliyoanzishwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

"Lengo letu ni kuonesha kuwa wanawake ni watu muhimu katika taifa letu kwani wao ndio walezi wakuu wa watoto nyumbani na kuhakikisha wanakuwa na maisha mazuri katika kuwalea watoto wao," alisema.

Hata hivyo alibainisha kuwa atandelea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa serikali kutoka 300,000 hadi 450,000.
 
Naye, Katibu Mkuu wa chama hicho Rashid Yussuf Mshenga alisema zoezi hilo limeanza rasmi jana na kudumu hadi Julai 7 mwaka huu kwa wanachama wanaotaka kugombea nafasi ya urasi wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho na Julai 8 wataanza kutoa fomu kwa ajili ya wanachama wanaotakia kugombea nafasi ya Udiwani, Uwakilishi na Ubunge.

Alisema ujumbe wa mwaka huu kwa chama hicho ni piga kura yako na kudumisha amani ya nchi yako kwani amani ni kitu muhimu kwa maendeleo ya watanzania.

Alisema, amani ni kitu muhimu kwa Tanzania kwani bila ya amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.

Hivyo, aliwaomba wananchi kujiunga na chama hicho na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo urasi kwani ndio mtaji muhimu katika kuendeleza chama chao.

Mbali na hayo alisisitiza vyama nyengine vya siasa kuendeleza dhana ya siasa safi iliyokuwepo Tanzania kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yao.