China yachukua udhibiti wa ubalozi mdogo wa Marekani huko Chengdu


Bendera ya Marekani imeshushwa katika ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Chengdu na maafisa wa China wakaingia katika jengo hilo. Haya yamejiri wakati ambapo China inajibu kwa njia ya vita baridi hatua ya Marekani kuufunga ubalozi wake huko Houston, Texas.

Mapema leo televisheni ya taifa ya China CCTV imeonyesha bendera hiyo ikishushwa baada ya mivutano ya kidiplomasia kuongezeka baina ya nchi hizo mbili huku kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kutishia usalama wa taifa lake.

 China baadaye imethibitisha kufungwa kwa ubalozi huo mdogo. Barabara inayoelekea ubalozi huo ulioko Chengdu imefungwa leo huku polisi wakionekana kulinda usalama.

Vyombo vya kitaifa vya habari China vinaripoti kuwa wafanyakazi katika ubalozi huo pia wameondoka mnamo saa kumi na mbili asubuhi.