Serikali ya mji wa Hong Kong inaweza kuahirisha kwa mwaka mmoja uchaguzi kwa ajili ya bunge la mji huo uliopangwa kufanyika Septemba 6 kutokana na kuongezeka kwa kesi za maambukizi ya virusi vya corona katika mji huo ambao ni kituo kikuu cha masuala ya kifedha duniani.
Kituo cha utangazaji mjini Hong Kong cha RTHK kimeripoti leo kikinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa.
Uchelewesho utakuwa pigo kwa jaribio la kambi ya upinzani inayopigania demokrasia kushinda wingi wa kutosha katika bunge la mji huo baada ya serikali ya China kuweka sheria mpya ya usalama ambayo imekosolewa kwa kiasi kikubwa na mataifa ya magharibi.
Wagombea wanaodai demokrasia zaidi walipata wingi mkubwa katika uchaguzi katika mabaraza ya chini ya ngazi ya wilaya mwaka jana.
