Katibu mkuu wizaraya kilimo ageuka mbogo ukamilishwaji maghalaya nafaka Makambako


Na Amiri Kilagalila,Njombe

Katibu mkuu wizara ya kilimo Gerald Kusaya amemuagiza meneja wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula mkoa wa Njombe na Iringa NFRA  pamoja na mhandisi mkazi wa TBA kumsimamia mkandarasi anaye jenga maghala  mawili ya  kuhifadhi  chakula mjini Makambako na kutaka maghala hayo  kukabidhiwa mapema mwezi Disemba mwaka huu.

Kusaya amechukua  uamuazi huo baada ya mkandarasi anaye jenga maghala hayo kusuasua kukamilisha ujenzi ambao mpaka sasa ulitakiwa uwe umekamilika na kuanza kuhifadhi nafaka mbalimbali  jambo ambalo limekuwa kinyume na makubaliano ya mkataba.

“Chukueni hatua TBA tunachotaka ikifika disemba 31 mimi nije hapa tarehe moja mwaka 2021 mnikabidhi majengo yangu hicho ndicho tunachotaka”alisema Kusaya

Awali kaimu meneja wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula mkoa wa Njombe na Iringa NFRA Frank Felix amesema mpaka sasa kanda hiyo yenye mikoa miwili ina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 22 na kuongeza kuwa ukasanyaji nafaka utaongezeka mara baada ya maghala mawili yanayo suasua kujengwa yakikamilika.

“Tumepangiwa jumla ya kununua tani elfu 30,ndani ya tani hizo tani elfu tano tutanunua mpunga na elfu 25 tutanunua mahindi,lakini maghala haya mawili yatakuwa na uwezo wa kuchukuwa tani elfu kumi kumi kwa hiyo jumla sasa ya mradi huu ni tani elfu 40”alisema Frank Felix

Akizungumzia changamoto za mradi wa ujenzi wa maghala mawili ya kuhifadhi  nafaka mhandisi mkazi wa TBA Eng.Pedon Mushobozi anasema uzembae wa mkandarasi,hali ya hewa pamoja na kusuasua kwa malipo,yamepelekea kuchelewa kukamilika kwa ujenzi huo.

“Changamoto kubwa hapa  ni malipo kwa mkandarasi  na imepelekea mkandarasi kuishiwa fedha”alisema Eng.Pedon Mushobozi

Katika hatua nyingine katibu mkuu wizara ya kilimo Gerald Kusaya amewataka wafanya kazi wote wanao fanya kazi chini ya wizara yake kujiendeleza kielimu kwani kufanya hivyo kunaongeza ufanisi kazini.