Klabu ya waandishi wa habari ya mkoa wa Lindi yapata safu mpya ya uongozi

 Na Ahmad Mmow, Lindi.

Klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Lindi(Lindi Regional Press Club) imepata viongozi wapya baada ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo kumaliza muda wao.

 Viongozi hao walipatikana jana kupitia uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Maendeleo uliopo katika manispaa ya Lindi.

Katika uchaguzi huo mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa kipindi kilichopita, Christopher Lilai alichaguliwa tena kushika wadhifa huo baada ya kupata kura 15 dhidi kura 11 alizopata mshindani wake, Josephine Kibiriti.

 Nafasi ya Katibu mkuu ilikwenda kwa Mwanja Ibadi aliyepata kura 17. Wakati Said Muunguja ambaye alikuwa anatetea nafasi hiyo aliambulia kura 9.

 Hadija Omari aliibuka mshindi na kutetea nafasi yake ya utunza hazina baada ya kupata kura 19 dhidi 8 alizopata Sofia Nyalusi.

 Aidha mgombea pekee wa nafasi ya umakamo mwenyekiti, Juma Mweru aliweza kutetea vema nafasi hiyo kwa kupata kura za NDIO 25,na kura 2 zikimkataa.

Huku nafasi ya naibu katibu mkuu ilichukuliwa na Ahmad Mmow ambaye hakuwa na mpinzani na kufanikiwa kupata kura zote 27.

 Akizungumza baada ya kutangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Stuart Lugongo alitoa wito kwa klabu za waandishi wa habari zijenge utamaduni wa kuanzisha miradi ya kiuchumi ili ziweze kujitegemea badala ya kutegemea misaada toka kwa wahisani na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC).

 Alisema klabu zikiwa na miradi ya kiuchumi zitakuwa na uwezo wa kujiendesha na kuendelea kuwa imara hata kama wahisani watashindwa kuzisaidia. Huku akiwakumbusha wanachama walipe ada. Kwani ni miongoni mwa vyanzo vya mapato.

 Christopher Lilai na Mwanja Ibadi ni waandishi wa gazeti la Mwananchi, Hadija Omari(Gazeti la Mtanzania), Juma Mweru(Ruangwa FM)