Mamilioni ya watu wakabiliwa na vizuizi vipya vya Corona

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na vizuizi vipya leo wakati maambukizi ya virusi vya corona yakiongezeka, lakini katika dalili moja ya matumaini, kampuni moja ya Kimarekani imesema itaanza hivi karibuni hatua ya mwisho ya majaribio ya chanjo ya ugonjwa huo.

Nchi nyingi duniani zimeweka upya hatua za kuwafungia watu kutoka nje pamoja na vizuizi ili kudhibiti maambukizi mapya, wakati idadi ya visa ulimwenguni ikipindukia milioni 13.2 na zaidi ya vifo 576,000.

Maeneo ya kanda ya Asia Pasifiki, ambayo kwa kiasi fulani yalikuwa yamefanikiwa katika kupambana na janga hilo, yalitoa ushahidi mpya wa kitisho kikubwa ambacho bado kinawekwa na kirusi hicho.

Kampuni ya Kimarekani ya Moderna imesema itaanza hatua ya mwisho ya majaribio ya chanjo yake Julai 27, baada ya kupata matokeo ya kutia moyo katika majaribio ya awali.

Kampuni hiyo inaongoza katika mbio za kutafuta chanjo ulimwenguni, na wakati utafiti wake ukipaswa kuendelea hadi Oktoba 2022, matokeo ya mwanzo yanatarajiwa kupatikana kabla ya muda huo.