Polisi Ujerumani yawakuta wahamiaji 31 wamejificha kwenye lori

Polisi na maafisa wa forodha nchini Ujerumani wamegundua wahamiaji 31 wakiwa wamejificha ndani ya lori moja ambalo lina jokofu karibu na mpaka wa Jamhuri ya Czech. Lori hilo lilisimamishwa jana usiku kwenye barabara kuu inayotoka kwenye mpaka wa mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Dresden.

Lilikuwa na nambari za usajili za Uturuki na pia lilikuwa limebeba matunda. Wahamiaji hao wote walikuwa wanaume na wenye umri wa kati ya miaka 18 na 47.

Shirika la habari la umma MDR limesema walitokea Syria, Uturuki, Iran na Iraq. Dereva wa lori hilo alikuwa raia wa Uturuki mwenye umri wa miaka 57 ambaye anazuiliwa na polisi.

Wahamiaji kadhaa wamefariki ndani ya malori katika kipindi cha miaka michache iliyopita wakati wakijaribu kuingia Ulaya. Wahamiaji 71 walifariki dunia ndani ya lori nchini Austria mwaka wa 2015, wakati mwaka wa 2019 wahamiaji 39 wa Vietnam walipatikana wamefariki kwenye lori nchini Uingereza.