Uingereza yaiwekea vikwazo Urusi na Saudia


Uingereza imewawekea vikwazo watu kadhaa pamoja na mashirika ya Urusi, Saudi Arabia, Myanmar na Korea Kaskazini kwa kukiuka haki za binaadamu.

 Tangazo hilo la Uingereza limetolewa baada ya nchi hiyo kupitisha sheria yake ya Magnitsky, ambayo inaruhusu mataifa kuwalenga raia wa kigeni au mashirika kutokana na kukiuka haki za binaadamu.

Marekani iliipitisha sheria hiyo mnamo mwaka 2012 kwa kumbukumbu ya Sergey Magnitsky,ambaye alikuwa mshauri wa masuala ya kodi aliyekufa akiwa kwenye gereza la Urusi katika mazingira ya kutatanisha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab amesema vikwazo hivyo vina lengo la kuzuia utakatishaji wa fedha.

Urusi imetishia kulipiza kisasi ikisema uamuzi huo wa Uingereza sio wa kirafiki. Uingereza inaweza kuitumia sheria hiyo kuwazuia kuingia nchini humo watu wanaoaminika kukiuka haki za binaadamu, pamoja na kuzuia mzunguko wa fedha katika mabenki.