UN yaonya kuhusu kupungua chanjo wakati wa janga la COVID

Viwango vya utoaji chanjo kwa watoto dhidi ya magonjwa hatari kama vile surua na pepopunda vimepungua kwa kiasi kikubwa wakati huu wa janga la COVID-19, hali inayowaweka mamilioni ya watoto katika hatari kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Afya, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika ripoti ya pamoja na Shirika la kuwashughulikia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF kuwa mateso na vifo vinavyoweza kuepukika ambavyo vinasababishwa na watoto kukosa kupewa chanjo za kila mara huenda vikawa juu zaidi ya vile vya COVID-19.

Karibu robo tatu ya nchi 82 zilizoshiriki kwenye utafiti wa ripoti hiyo zilisema mipango yao ya utoaji chanjo ilivurugika kutokana na virusi vya corona kufikia Mei 2020. Kwa mujibu wa WHO, milipuko ya surua ilikuwa tayari imeongezeka, kwa kuwaambukiza karibu watu milioni 10 katika mwaka wa 2018 na kuwauwa 140,000 wengi wao watoto.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items