Upinzani Mali wakataa makubaliano na Rais Keïta huku kukiwa na maandamano makubwa


Viongozi wa upinzani nchini Mali wamemtaka rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu , baada ya kukataa makubaliano yaliolenga kuzuia machafuko yanayoendelea nchini humo.

Takriban watu wanne waliuawa wakati wa maandamano siku ya Ijumaa , na kulikuwa na makabiliano zaidi siku ya Jumamosi.

Maandamano hayo yalimlazimu rais kufutilia mbali mahakama kuu ambayo imekuwa katikati ya mgogoro huo baada ya kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi mwezi Machi.

Lakini muungano wa upinzani ulikataa pendekezo lake muda mfupi baadaye.

Umati mkubwa wa waandamanaji wamtaka rais wa Mali kujiuzulu - kunani?
Je wajua mtu tajiri zaidi duniani alikuwa Mwafrika?
Nouhoum Togo, msemaji wa kundi la M5-RFP la viongozi wa kidini pamoja na wanasiasa ambalo liliandaa maandamano ya hivi majuzi amesema kwamba 'hatuwezi kukubali upuzi huu'.

''Tunataka ajiuzulu mara moja'' , aliambia chombo cha Reuters siku ya Jumapili.

Wapinzani hawafurahii jinsi rais Keita anavyolisimamia suala la wapiganaji wa Kijihad , mzozo wa kiuchumi na uchaguzi huo ambayo matokeo yake yanapingwa.

Imam wa kihafidhina Mahmoud Dicko anaongoza muungano wa upinzani.

Amekuwa akisisitiza kuwepo kwa mabadiliko zaidi baada ya kukataa makubaliano ya awali kutoka kwa rais huyo ikiwemo kubuniwa kwa serikali ya Umoja.

Siku ya Jumapili, bwana Dicko alitoa wito wa kuwepo kwa utulivu na kusema atatoa hotuba katika runinga baadaye siku hiyo.

''Tulia ,Tulia'' , alisema kulingana na chombo cha habari cha AFP.

''Tunaweza kupata tunalopigania kupitia subra na tabia nzuri''.

Watu wanne walifariki katika maandamano ya siku ya Ijumaa mjini Bamako , kulingana na maafisa. Kulikuwa na vifo vinne zaidi siku ya Jumamosi.

Je rais huyo alikubali kufanya nini?
Huku maandamano yakiendelea siku ya Jumamosi , rais alitoa hotuba ya jioni , akisema ataivunjilia mbali mahakama ya kikatiba.

''Nimeamua kufutilia mbali leseni za wanachama wa mahakama hiyo waliosalia'' , alisema.

''Kufutiliwa mbali kwa mahakama hii kutasaidia …wahusika kuwachagua wanachama wapya ili mahakama hiyo iliofanyiwa mabadiliko iweze kutusaidia mara moja kutafuta suluhu ya makosa yaliofanyika katika uchaguzi huo wa wawakilishi wa bunge'', aliongezea.

Rais Keïta alipendekeza kwamba anaweza kukubali kurudiwa kwa uchaguzi katika baadhi ya mabunge , suala ambalo ni miongoni mwa mahitaji ya waandamanaji hao. Hili lilipendekezwa mwezi uliopita na shirika la mataifa la Afrika magharibi Ecowas.

Akizungumza mapema siku ya Jumamosi , waziri mkuu Boubou Cisse alisema kwamba yeye na rais walikuwa tayari kufanya mazungumzo na kuahidi kubuni serikali itakayowajumuisha wadau wote 'haraka iwezekanavyo'.

Makubaliano hayo yalijiri huku upinzani ukisema kwamba vikosi vya usalama vilikuwa vikiwazuia viongozi wawili waliokuwa wakiandamana , Choguel Kokala Maiga na Moutaga Tall.

Kiongozi mwengine wa maandamano hayo Issa Kaou Djim alikamatwa siku ya Ijumaa.

''Vikosi vya usalama pia vilikuwa vikipekua makao yetu makuu'' , msemaji wa muungano wa upinzani Nouhoum Togo alisema.

Kiongozi wa mojawapo wa vyama vya upinzani , Yeah Samake aliambia BBC kwamba alikataa ombi la bwana Keita na kumtaka ajiuzulu.

''Tunataka rais ajiuzulu kwasababu amefeli Mal''i , aliambia kipindi cha NewsHour.

''Hakufanya aliyowaaahidi watu wa Mali, kupigana na ufisadi, kutoa ajira kwa vijana na haya ndio mahitaji ya raia wa Mali''.