Hong Kong yaahirisha uchaguzi kwa sababu ya Corona


Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam ametangaza kuahirishwa uchaguzi wa bunge uliokuwa ufanyike Septemba 6. Lam ameleeza kwamba uchaguzi huo umeahirishwa kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya wajumbe 12 wa upinzani kukataliwa kugombea katika uchaguzi huo. Wajumbe hao ni pamoja na kiongozi wa harakati za kidemokrasia Joshua Wong.

Wong ameeleza kuwa serikali ya China inachukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuwazuia wapinzani kushinda viti vingi bungeni.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema nchi yake itasimamisha kwa muda utekelezaji wa mkataba, baina ya Ujerumani na Hong Kong unaowezesha wahalifu wa kila upande kurudishwa kwao.

Maas amesisitiza kwamba Ujerumani wakati wote inatarajia kuwa China ambayo imetangaza sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hong Kong itatekeleza wajibu wake wa kimataifa.