Malawi yatangaza vizuizi vipya vya kukabiliana na janga la virusi vya corona

Malawi leo imetangaza kuyafunga makanisa yote na kumbi za starehe katika awamu mpya ya vizuizi vya kudhbiti ongezeko linalotia wasiwasi la virusi vya corona.

Vizuizi vipya vilivyotangazwa kupitia gazeti la serikali vinajumuisha pia amri ya kuvaa barakoa na marufuku kwa mikusanyiko inayozidi watu 10 isipokuwa kwa shughuli za mazishi zitakazoruhusu jumla ya watu 50.

Mwanasheria Mkuu wa serikali Chikosa Silungwe amesema kikosi maalum cha maafisa wa jeshi kimeundwa kuhakikisha masharti hayo mapya yanatekelezwa. Malawi haijatekeleza marufuku kamili ya shughuli za umma baada ya mahakama kuzuia mwezi April nia ya serikali ya kuifunga nchi nzima kwa sababu ilishindwa kutangaza msaada utakaotolewa kwa watu wasiojiweza.

Tangu taifa hilo la kusini mwa Afrika lilipotangaza kisa cha kwanza cha COVID-19 mnamo Aprili 2, idadi ya maambukizi imepanda maradufu katika kipindi cha wiki nne zilizopita na kufikia visa 4,624 ikiwemo vifo 143.