https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mashabiki wa Liverpool Dodoma washeherekea EPL kwa kukabidhi msaada kwa wenye uhitaji | Muungwana BLOG

Mashabiki wa Liverpool Dodoma washeherekea EPL kwa kukabidhi msaada kwa wenye uhitaji


KATIKA kusheherekea ubingwa wa Ligi Kuu ya England mashabiki wa Liverpool jijini Dodoma, wametembelea Kituo cha watoto wenye uhitaji cha Kijiji cha Matumaini na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto hao.

Katika tukio hilo mashabiki hao wameongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira, Anthony Mavunde ambaye amewataka mashabiki wa timu zingine ikiwemo za hapa nchini kuwa na moyo wa kusaidia watu wenye uhitaji.

Naibu Waziri Mavunde amesema licha ya yeye kuwa shabiki wa Manchester United ambao ni wapinzani wa Liverpool lakini ameguswa kuungana na mashabiki hao kutokana na moyo wao wa kusheherekea furaha yao kwa kupeleka mahitaji mbalimbali kwa watoto hao.


" Niwapongeze sana ndugu zangu wa Liverpool kwa moyo wenu wa upendo, mngeweza kuchanga fedha zenu na mkafanya sherehe kwa kunywa pombe lakini mmeona ni vema mlete mahitaji kwa watoto hawa, Mungu awabariki na iwe rai kwa mashabiki wa timu zingine kufanya tukio la kizalendo kama hili," Amesema Mavunde.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mashabiki hao, Abraham Gama amesema wao kama mashabiki wameona washeherekee ubingwa wao kwa kuwaletea watoto hao mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, pampers, mafuta ya kupikia, sabuni, nguo na maziwa ambayo yote ina gharama ya Sh Milioni Moja.

Nae Katibu wa Mashabiki hao, Charles James amewashukuru wadau mbalimbali waliojitolea kufanikisha tukio hilo ikiwemo Kampuni ya Matairi ya Binslum Tyres na Kampuni ya Maziwa ya Tanga Fresh.

" Hili ni tukio endelevu na tumepanga uwe utaratibu wa mashabiki wa Liverpool Dodoma kusaidia watu wenye uhitaji mara kwa mara, Liverpool ni Klabu inayothamini utu na yenye kujali watu wenye uhitaji tutaendelea kusaidia wenye uhitaji hata bila kusubiri kutwaa ubingwa," Amesema James.