Na John Walter-Babati, Manyara
Jioni ya kawaida mjini Babati, kundi la wanaume lilikuwa
limekusanyika kuangalia mpira.
Vicheko na kelele za shangwe vilitawala hewani, hadi pale
ghafla hali ilipobadilika.
Mwanaume mmoja alisimama kwa taharuki, akapiga kelele kwa
sauti ya hofu: “Nyeti zangu zimepotea!”
Ndani ya sekunde chache, furaha ilitoweka.
Watu wakasogea kwa taharuki, wengine wakaanza kukimbia, huku
macho yakianza kumtafuta mtu wa kulaumiwa.
Kilichoanza kama dai la mtu mmoja kiligeuka kuwa hofu ya
pamoja—hofu iliyosambaa kwa kasi kama moto wa nyika.
Matukio kama hayo yameendelea kujirudia katika maeneo
mbalimbali nchini, yakichochewa na taarifa za uzushi zinazosambaa mitandaoni
kuwa mwanaume akiguswa begani hupoteza sehemu zake za siri.
Kwa mujibu wa David Misime,msemaji wa jeshi la polisi nchini, ndani ya siku nne pekee, watu saba walipoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa baada ya wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watu waliotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo.
Anasema uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa madai hayo hayana
ukweli wowote, kwani waliodai kupoteza sehemu zao walikutwa nazo, jambo
linaloonyesha wazi kuwa hofu hiyo inachochewa na imani potofu na uvumi usio na
msingi.
Wakati mamlaka zikijaribu kuzima taharuki hiyo, taarifa hizo
zinaendelea kusambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, zikiwafikia watu
wengi ndani ya muda mfupi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameonya kuwa taarifa hizo ni za upotoshaji na zinachochea hofu isiyo ya lazima katika jamii, akizitaka jamii kuzipuuza na kutozieneza.
Lakini kwa wananchi kama Mbaraka Sungi, tukio
alilolishuhudia bado linamkaa akilini.
Anasema siku hiyo alipokuwa akiangalia mpira, mwanaume mmoja
alisimama ghafla na kuanza kupiga kelele kuwa amepoteza nyeti zake baada ya
kushikwa bega.
Watu walimzunguka kwa mshangao na hofu, huku hali ya
sintofahamu ikitawala eneo hilo. “Ilikuwa hali ya kutisha sana,” anasema,
akiongeza kuwa baada ya tukio hilo, wanaume wengi walianza kuishi kwa hofu,
wakihofia hata kuguswa na watu wengine.
Hofu hiyo inaungwa mkono na kauli za baadhi ya wananchi
wanaoona kuwa uvumi huo umevuka mipaka na kuwa tishio kwa usalama wa jamii.
Lucas Mondu anasema si jambo la kulifumbia macho,
akisisitiza kuwa wanaosambaza propaganda hizo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.
Naye Rose Njate anasema alishuhudia taarifa hizo zikisambaa kwa kasi mitandaoni, hali iliyochochea taharuki na hofu miongoni mwa wananchi.
Kwa mtazamo wa kitaalamu wa kidini, Clemence Matwiga
anaeleza kuwa imani potofu huota mizizi katika ukosefu wa elimu sahihi ya
kiimani na uelewa mdogo wa mambo ya msingi.
Anasema jamii inapokosa maarifa sahihi, huwa rahisi kuamini
jambo lolote linaloibua hofu, hata kama halina ushahidi wa ukweli.
Hali hiyo, anaonya, inaweza kusababisha watu kuchukua hatua
za haraka na za hatari dhidi ya wenzao.
Mtazamo huo unaungwa mkono na viongozi wa kimila, akiwemo
Chifu Dodo Zuberi Sige Chifu wa Wagorowa , ambaye anasema baadhi ya watu
wameanza kupotosha mila na kuziingiza katika vitendo visivyo na msingi.
Anasisitiza kuwa mila halisi hazihusiani na ukatili au
mauaji, bali kinachoonekana sasa ni kupotoka kwa maadili na matumizi mabaya ya
imani za jadi.
Katika muktadha huu, matukio ya kushambuliwa na kuuawa kwa
watu wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo yanaibua taswira ya jamii
inayosukumwa na hofu kuliko ukweli.
Uvumi unapoanza, huzalisha hofu; hofu huzalisha hasira; na
hasira, mara nyingi, huishia katika vurugu na mauaji ya watu wasio na hatia.
Jeshi la Polisi pia limeeleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa
wakisambaza taarifa hizo kwa makusudi, hata kwa njia ya vichekesho, ili kuvutia
wafuasi katika mitandao ya kijamii.
Kitendo hicho, kwa mujibu wa mamlaka, si tu kinachochea hofu
bali pia kinachangia moja kwa moja madhara yanayoikumba jamii.
Kadri teknolojia inavyorahisisha mawasiliano, ndivyo pia
inavyorahisisha kusambaa kwa taarifa za uongo.
Katika mazingira haya, mstari kati ya ukweli na uzushi
unazidi kuwa mwembamba, na madhara yake yanabebwa na wananchi wa kawaida.
Swali linalobaki ni je, jamii itaendelea kuamini kila
kinachosikika bila kuthibitisha, au itachagua kusimama upande wa ukweli na
kulinda maisha ya watu?




0 Maoni