Na Linda Mosseka-Manyara
Watoto ni taifa la kesho, msemo huu umezoeleka masikioni mwa
wengi ukiwa umebeba maono makubwa ya maisha ya watoto wa kitanzania katika
kuwaandaa kuwa watu muhimu kwenye jamii pale wanapofikisha umri wa utu uzima,
ili waweze kulisaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo kwa kutumia ujuzi,
maarifa na vipaji walivyonavyo.
Mara nyingi mchakato wa watoto kuzifikia ndoto zao hukumbwa
na mambo mengi mazito ikiwemo changamoto ya kiuchumi, maradhi na kubwa zaidi ni
ukatili wanaofanyiwa kwenye jamii inayowazunguka hasa wazazi na ndugu wengine
wakaribu wanaowategemea.
Kutokana na changamoto ya ukatili kuongezeka nchini kwa
kiwango kikubwa, wadau mbalimbali kwa kushirikiana na serikali waliguswa
kuwasaidia watoto wanaopitia changamoto mbalimbali kwa kuandaa vituo maalum vya
malezi ili kuhakikisha wanafikia ndoto
zao.
Utaratibu wa kuanzisha vituo hivyo unasimamiwa na wizara ya
maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum, kuanzia kwenye usajili na
kuratibu namna vituo hivyo vinavyoendeshwa.
Vituo hivi ni vya binafsi, vinasajiliwa kama mashirika
yasiyo ya kiserikali chini ya sheria inayosimamia mashirika hayo ya mwaka 2002
kifungu cha 56 na marejeo yake.
Katika makala hii tunaangazia ni kwa namna gani vituo hivyo
vya kulelea watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu vimesaidia
kupunguza ukatili kwa watoto, ambatana nami kuanzia mwanzo hadi tamati ya
makala hii jina langu ni Linda Moseka.
Kwa mujibu wa sheria za nchi ikiwemo katiba ya jamhuri ya
muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 zinaweka
bayana kuwa mtoto ni binadamu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, na
anastahili haki za msingi kama binadamu wengine ikiwemo haki ya kuishi,
kulindwa kupata malezi bora, elimu na afya bora.
Kila kukicha nchini Tanzania na duniani kwa ujumla
kumeripotiwa matukio mbalimbali ya ukatili dhidi ya watoto yanayopelekea watoto
kushindwa kupata haki zao za msingi na badala yake wanajikuta kwenye dimbwi la
mateso na manyanyaso yanayosababisha msongo wa mawazo na kupelekea kufanya maamuzi magumu ikiwemo kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa tafiti za shirika la afya duniani WHO
takribani watoto bilioni moja wenye umri wa miaka 2-17 hupitia aina mbalimbali
za ukatili kila mwaka ikiwemo ukatili wa kisaikolojia, kutokana na adhabu kali
kutoka kwa wazazi au walezi wao.
Kwa upande wa tafiti za shirika la umoja wa mataifa la
kuhudumia watoto UNICEF 2025 zimeonesha kuwa watoto 6 kati ya 10 wenye umri wa
miaka 2-14 hupitia ukatili wa kisaikolojia
wakiwa nyumbani ikihusisha kutukanwa, kufokewa kwa ukali au
kudhalilishwa na wazazi au walezi wao.
Ripoti hiyo imeendelea kuonesha kuwa bara la Afrika ni
miongoni mwa maeneo yenye viwango vya juu zaidi vya tatizo hili kwani takribani
asilimia 80 ya watoto hupitia adhabu za vurugu nyumbani zinazojumuisha
vipengele vya ukatili wa kisaikolojia na kimwili.
Nchini Tanzania utafiti wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto (VACS) wa mwaka
2024 ulionesha takribani asilimia 25 ya wasichana na asilimia 31 ya wavulana
walipata ukatili wa kisaikolojia kutoka kwa watu wazima kabla ya kufikisha
miaka 18.
Mtiririko wa ripoti hizi unaonesha wazi kuwa bado changamoto
ya ukatili kwa watoto katika jamii ni kubwa na mikakati ya ziada inahitajika
ili kuhakikisha ukatili unatokomezwa, ikiwa sambamba kabisa na sheria ya mtoto
ya mwaka 2009 na marejeo yake ya mwaka 2019, ambapo kifungu cha 13 kinakataza
mtu yeyote kumtesa mtoto au kumfanyia adhabu nyingine ya kikatili, isiyo ya
kibinadamu au inayodhalilisha utu wake.
Moja ya njia madhubuti ambayo serikali ya jamhuri ya
muungano wa Tanzania pamoja na wadau wameamua kuitumia ili kupunguza ukatili
kwa watoto ni kuanzisha vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye
mazingira magumu, vituo hivi vinaendeshwa kwa uangalizi wa serikali na misaada
ya wadau binafsi na wafadhili.
Nchini Tanzania kuna takribani mashirika 8,959 yasiyo ya
kiserikali yaliyosajiliwa, yanayohudumu katika sekta mbalimbali za maendeleo ya
jamii kama afya, elimu, haki za binadamu na ustawi wa watoto.
Mashirika yaliyojikita kufanya kazi katika masuala ya
maendeleo na ustawi wa mtoto nchini Tanzania hadi kufikia mwaka 2025 ni
takriban mashirika 142.
Katika mkoa wa Manyara kuna takribani vituo saba (7) vinavyolea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu, moja kati ya vituo hivyo ni kituo cha Hossana Home Care Foundation kilichopo mtaa wa Nyawari, kata ya Singe wilayani Babati mkoani Manyara.
Nimepata fursa ya kutembelea kituo hicho ili kujionea
maendeleo ya watoto wanaolelewa katuoni hapo, na kwa hakika nimekutana na
watoto wenye nyuso nzuri za matumaini zilizojawa na tabasamu zinazoashiria
kwamba wapo sehemu salama.
Nakutana na binti shupavu, mwenye kujiamini aliyebeba
hadithi ya kusisimua kwa mapambano magumu aliyopitia yaliyomfanya kukataa tamaa
hadi pale tumaini jipya lilipoingia baada ya kupata nafasi ya kulelewa katika
kituo hicho.
Binti huyu anatambulika kwa jina la Doreen Dastan mwanafunzi
wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Ft Sumaye, Doreen anasimulia
hadithi ya kusisimua ya maisha yake iliyomfanya apitie changamoto ya ukatili wa
kisaikolojia kutoka kwa baba yake mzazi, kwani suala la ugomvi baina ya Baba na
Mama ilikuwa ni maisha ya kawaida sana kwao, achilia mbali maisha duni ya
familia.
Doreen anasema aliishi maisha ya kufokewa, kutukanwa na hadi kupelekea kuwa na msongo mkubwa wa mawazo akitafakari ni lini ataipata amani kwani alikosa tumaini kabisa na hali ikawa mbaya zaidi baada ya wazazi kutengana, mama yake aliamua kuhama kutoka Morogoro na kuhamia mjini Babati baada ya kushindwa kuvumilia maisha ya manyanyaso na vipigo kwake na kwa watoto wake.
"Baba yangu hakuwa mlevi bali alikuwa mtu mkorofi sana,
licha ya ugumu wa maisha tuliokuwa nao lakini ugomvi usiokwisha nyumbani
ilikuwa ni changamoto nyingine kubwa kwangu, nilitamani maisha ya amani na
utulivu na hata uamuzi wa mama kuhama kutoka Morogoro kuja Babati uliongeza
changamoto nyingine, kwani changamoto za magonjwa kwa mama zilikuwa nyingi na
hatukuwa na pesa, na iliniongezea mawazo zaidi kwakuwa nilikosa tumaini la
kusonga mbele". Ameeleza Doreen.
Licha ya changamoto hizo, ndoto ya kupata elimu kwa Doreen
haikufa kwani aliendelea kujitahidi kwenda shule huku Mama yake akifanya
jitihada za kutafuta msaada huku na kule kwa kushirikiana na ndugu na ndipo
tumaini jipya likatokea baada ya kupata nafasi ya kulelewa katika kituo cha
kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu cha Hossana Home
Care Foundation.
Doreen anasema ilikuwa furaha kubwa sana kwake kwenda kuanza
maisha mengine ya utulivu na amani akiamini kutimiza ndoto zake za kuwa
Mwandishi bora wa habari hapa nchini, na kwa sasa anakiri kupata utulivu wa
akili kwani anaishi vizuri na anapata mahitaji ya msingi kama mtoto na hatamani
kabisa kurudi kwa baba yake kwa kuhofia aliyoyapitia.
"Mama yangu ni fundi cherehani lakini kipato chake
kilikuwa kidogo sana hata kodi ya nyumba alishindwa kulipa, ndipo kwa
kushirikiana na Mama yangu mkubwa wakaamua kunitafutia msaada ili nimpunguzie
mzigo wa mahitaji ya shule na ndipo nikapata nafasi kwenye kituo hichi ambacho
kwakweli nimefurahi sana kwani ninaishi vizuri na nina amani hata msongo wa
mawazo umeisha, naamini kwa hapa nilipo nitatimiza ndoto zangu za kuwa
Mwandishi bora wa habari". Ameongeza Doreen.
Kwa sasa Doreen anafurahi kukutana na marafiki wapya katika kituo hicho akiwemo rafiki yake kipenzi Mwanaisha Juma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Balang'dalalu, na kwa pamoja wanapambania ndoto zao, japo hadithi ya Mwanaisha iligubikwa zaidi na changamoto ya kiuchumi kwa familia yake kiasi cha kupata mlo mmoja tu kwa siku na jitihada zake binafsi zikamfanya kupata fursa hii baada ya kueleza changamoto yake kwa Mwalimu mkuu na kumuombea nafasi ya kulelewa kituoni hapo, kwa pamoja wanaamini kufanikiwa kwani wanafundishwa maadili mema na namna ya kukabiliana na changamoto.
"Mimi nilikuwa napata mlo mmoja tu kwa siku, hata
shuleni nilikuwa sili kwakuwa wazazi walishindwa kulipia chakula, ndipo
nikaamua kuzungumza na mwalimu mkuu ili aweze kunisaidia, na ninamshukuru sana
kwani alinisaidia kuniombea nafasi kwenye kituo hichi cha Hossana na kwasasa
naishi hapa nimepata marafiki kama Doreen na tunaamini tutatimiza ndoto
zetu". Ameeleza Mwanaisha Juma rafiki yake Doreen Dastan
Kwenye vituo hivi vya kulelea watoto yatima na wanaoishi
kwenye mazingira magumu wapo wasimamizi wanaoishi na watoto na kuwahudumia
mahitaji yao ya msingi ya kilasiku, ndivyo ilivyo pia katika kituo cha Hossana
yupo mwanadada anayetambulika kwa jina la Annagress Justin anayefanya kazi ya
kuwahudumia na kuwafundisha mambo mbalimbali ya kimaadili.
Annagress anasema ameanza kazi katika kituo hicho tangu
mwaka 2021 na amewapokea watoto wengi ambao baada ya kufika katika kituo hicho
walionesha mabadiliko makubwa ikiwemo kuwa na afya njema na furaha, kwani
watoto wengi walikuwa wamedhoofu na wanamsongo mkubwa wa mawazo kutokana na
yale waliyopitia huko nyumbani.
Ukiachilia mbali chakula na malazi Annagress anasema wanafundisha maadili na kumjua Mungu kupitia dini zao ili wafuate yale ambayo mwenyezi Mungu anaamuru kupitia vitabu vyake vitakatifu na zaidi kabisa ni kuhusu stadi za maisha kwani wanafanya kazi mbalimbali za mikono ikiwemo kupika, kuosha vyombo, kutunza bustani na kulima, yote haya ni kwa lengo la kuwajengea uimara wa kimwili na kiakili na kuujua uhalisia wa maisha na nafasi zao katika jamii na wanashirikiana vyema na maafisa ustawi ikiwemo kuwaletea miradi ya kuku na mbuzi.
"Watoto wengi wanaokuja hapa changamoto zao kubwa huko
nyumbani ni wazazi kuwa walevi, akija nyumbani hamjali tena kama mtoto, ni
kumchapa na adhabu nyingine zisizostahili, sisi kwanza sheria yetu ni kilasiku
lazima tuungane pamoja na tusali, lakini pia siku za ijumaa kwa waislamu
wanaenda msikitini na wakristo jumapili kanisani na pia tunawafundisha shughuli
za mikono na tunamiradi ya kuku na mbuzi". Amesema Annagress mlezi wa
watoto.
Annagress anasema wapo watoto wengi wenye uhitaji lakini wao
kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii wanawasidia kufuatilia kwenye
maeneo yao ili kugundua kama kuna watoto wenye changamoto na wanaandika barua
ya kuomba nafasi ya malezi.
"sisi tunaletewa na maafisa ustawi wa jamii, afisa
ustawi baada ya kujua changamoto ndiyo anamleta hapa na atapiga simu kuomba na
tunashirikiana nao vizuri".Ameongeza Annagress mlezi wa watoto kituoni
hapo.
Matokeo ya utafiti wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto
Tanzania (VACS) umeonesha kupungua kwa ukatili wa kisaikolojia, kwa wasichana
umepungua kutoka 25% mwaka 2009 hadi kufikia 22% mwaka 2024 na kwa wavulana
umepungua kutoka 31% mwaka 2009 hadi kufikia 16% mwaka 2024.
Takwimu hizi zinasadifiwa na maelezo ya afisa ustawi wa
jamii wa Halmashauri ya mji wa Babati Agatha Patrice, ambaye amekiri kuwa uwepo
wa vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu
umesaidia kupunguza ukatili kwa watoto.
"Tunaona wazi kuwa vituo vimetusaidia kutulelea watoto
na vimesaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto,
kwani watoto wengi wanatoka kwenye familia zenye migogoro ya muda mrefu
inayopelekea hata wazazi kuachana na kuwafanya watoto waishi katika mazingira
magumu ya msongo wa mawazo kwasababu hakuna amani na utulivu nyumbani".
Ameeleza Agatha Patrice afisa ustawi wa jamii halmashauri ya mji wa Babati.
Afisa ustawi Agatha Patrice ameongeza kuwa kwa sasa
wanaendelea na jitihada za kubaini watoto wenye changamoto za ukatili kwenye
jamii kwa kutumia utaratibu wa kupata taarifa mbalimbali kutoka kwenye mitaa na
kata na kupitia kwa watu wanaoona familia zenye changamoto na watoto
wanaothirika kama mabalozi na wenyeviti wa mitaa, na mara nyingi huwa wanafika
ofisini na baada ya hapo wanaanza kufatilia na wakibaini huandika barua kwenye
vituo kuomba nafasi.
"Utaratibu ambao tunautumia ni kupata taarifa
mbalimbali kutoka kwenye kata na mitaa kupitia kwa watu wanaoona kabisa kwamba
familia fulani watoto wanaathirika au kwa mabalozi na wenyeviti wa mitaa,
kwahiyo tunavyopata hizo taarifa kama halmashauri tunachukua hatua ya kufika
kwenye eneo husika tutawakuta hao watoto, tutaongea na majirani, tutamtafuta
mzazi na tukijiridhisha tunaandika barua ya maombi kwenye hizi taasisi za
kulelea watoto na tunawapeleka". Ameongeza Agatha Patrice afisa ustawi wa
jamii halmashauri ya mji wa Babati.
Ushirikiano mzuri baina ya maafisa ustawi wa jamii na vituo
vya kulele watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kiasi kikubwa
unaonekana kusaidia ustawi wa watoto kwenye jamii kwani mazingira bora, amani
na utulivu ni nyenzo kubwa sana za kumupeusha mtoto na ukatili.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri kutoka chuo
kikuu cha Iringa kitivo cha Saikolojia Robert Lwiza anasema maendeleo ya mtoto
huletwa na amani na utulivu, ambavyo vinamsaidia mtoto kujenga akili yenye
afya, hisia zilizo imara, kujiamini na uwezo mzuri wa kujifunza na kuhusiana na
wengine.
"Amani na utulivu humsaidia mtoto kujenga akili yenye
afya, kujiamini, hisia zilizo imara na uwezo wa kuhusiana na wengine na
kujifunza na hata uwezo kuzikabili changamoto na ndio maana huwa tunasisitiza
sana umuhimu wa mazingira salama, yenye upendo na yasiyo na migogoro mikubwa
katika malezi ya mtoto ili aepukane na ukatili wa kisaikolojia".Amesema
Mwanasaikojia Robert Lwiza.
Mafanikio haya ya kupunguza ukatili kwa watoto yanakwenda
sambamba na juhudi za wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi
maalumu, inayoongozwa na mwanamama shupavu Dkt Dorothy Gwajima ambayo
inasamimia sheria, sera na miongozo mbalimbali inayohusu ustawi wa watoto hapa
nchini Tanzania.
Na mara kadhaa kupitia majukwaa mbalimbali ametoa wito kwa jamii kuacha ukatili kwa watoto na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuwafundisha watoto bila kuwaletea madhara.
"Wapendwa walezi na walimu wa watoto wetu mashuleni,
pamoja na kazi nzuri mnayofanya hima zingatieni kulea watoto pasipo kuwaletea
madhara ya adhabu zilizo nje ya mwongozo, vinginevyo mtaendelea kuhatarisha
ustawi wa watoto". Alisema Dkt Dorothy Gwajima waziri wa maendeleo ya
jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu.
Kwasasa Doreen Dastan anamatumaini makubwa ya kutimiza ndoto zake za kuwa mwandishi bora wa habari ili aisaidie jamii kupaza sauti juu ya mambo ya ukatili na kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama na anaiomba serikali na wadau binafsi waendelee kuwashika mkono ili waendelee kusonga mbele.
Ama hakika mwanzo wa ngoma ni lele na hakuna marefu yasiyo
na ncha na kufikia hapa ndio tamati ya makala hii, iliyoangazia ni kwa namna
gani vituo vya kulele watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu
vinavyosaidia kupunguza ukatili kwa watoto, bila shaka umejifunza mengi, hadi
wakati mwingine jina langu ni Linda Moseka.







0 Maoni