NA REBECA DUWE TANGA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeomba kuendelea kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland kupitia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Maziwa Faida kuanzia mwaka 2027 hadi 2032, ili kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuimarisha uzalishaji wa maziwa, kuongeza tija na kuboresha maisha ya wafugaji nchini.
Ombi hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Madele, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026) yaliyofanyika katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki, jijini Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Madele amesema Mradi wa Maziwa Faida unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TALIRI na Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na Chakula ya Ireland (TEAGASC), kwa ufadhili wa Serikali ya Ireland kupitia Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya maziwa, hususani katika Mkoa wa Tanga.
Dkt. Madele amesema kabla ya kuanza kwa mradi huo, wafugaji wengi walikuwa wakizalisha wastani wa lita 3 hadi 5 za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku. Kupitia matumizi ya teknolojia bora za ufugaji, malisho bora, huduma za ugani zilizoimarishwa na mafunzo kwa wafugaji, uzalishaji umeongezeka hadi wastani wa lita 15 kwa ng’ombe mmoja kwa siku katika maeneo mengi yaliyofikiwa na mradi.
“Matokeo haya yanaonesha wazi mchango mkubwa wa utafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa katika kuongeza tija, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini,” alisema Dkt. Madele.
Aidha, Dkt. Madele amesema kuwa Tanzania kwa sasa inazalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, wakati mahitaji ya taifa yanakadiriwa kufikia lita bilioni 13 kwa mwaka, amesema hali hiyo inaonesha uwepo wa fursa kubwa ya kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa maziwa ili kupunguza pengo la mahitaji na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Suzanne Keatinge, ameipongeza TALIRI kwa utekelezaji mzuri wa Mradi huo na kuwatambua watafiti, wataalamu wa ugani na wadau wote waliochangia mafanikio ya mradi huo.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba, ameishukuru Serikali ya Ireland kwa ufadhili wake na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maziwa Faida (2021/2022–2025/2026) yameweka msingi imara wa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya maziwa nchini.
Prof. Komba alisema TALIRI itaendelea kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti, ubunifu na teknolojia zilizozalishwa kupitia mradi huo zinawafikia wafugaji wengi zaidi nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa sekta ya maziwa.
Aliongeza kuwa Mradi wa Maziwa Faida, uliogharimu zaidi ya Euro milioni 3 sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 7 za Kitanzania, umenufaisha zaidi ya wanawake na vijana 3,000 katika ukanda wa pwani ya mashariki, hususan Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Prof. Komba, mafanikio makubwa ya mradi huo ni pamoja na kufanya tafiti za malisho bora yanayostahimili mazingira ya ukanda wa pwani, kubaini aina bora za ng’ombe wa maziwa, kuwajengea uwezo maafisa ugani, kutoa mafunzo kwa wafugaji, kuimarisha vyama vya ushirika vya wafugaji, kuboresha miundombinu ya utafiti pamoja na kuanzisha mashamba darasa ambayo yamekuwa vituo muhimu vya kujifunzia na kusambaza teknolojia za kisasa za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Mradi wa Maziwa Faida unatajwa kuwa mfano bora wa ushirikiano wa maendeleo unaochochea matumizi ya utafiti na ubunifu katika kutatua changamoto za uzalishaji wa maziwa na kuchangia ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo nchini Tanzania.




0 Maoni