https://monetag.com/?ref_id=TTIb Masoko ya madini ya vito na dhahabu Ruvuma yaingiza zaidi ya bilioni 5.5 | Muungwana BLOG

Masoko ya madini ya vito na dhahabu Ruvuma yaingiza zaidi ya bilioni 5.5

Na Muhadh Mohammed. Songea  Ruvuma.
Masoko  ya madini ya vito na dhahabu mkoani Ruvuma tangu kufunguliwa kwake Mei 2019 hadi kufikia Mei 2020 yamenunuliwa madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.5.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema katika kipindi hicho masoko hayo yaliopo Tunduru na Songea yamewezesha kununuliwa  madini yenye uzito wa gramu  390,936.27.

“Mrabaha uliopatikana katika mauzo hayo ni shilingi  milioni 332,093,674.35,ada ya ukaguzi iliyopatikana ni shilingi milioni 55,348,945.72 na kodi ya huduma iliyopatikana katika kipindi hicho ni shilingi milioni 16,604,683.72’’,alisema Mndeme.

Mndeme amesema serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli imeendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa ajili ya kukuza Sekta ya Madini katika Mkoa wa Ruvuma.

Amesema sekta ya Madini Mkoa wa Ruvuma imekuwa kwa kasi katika maeneo ya uwekezaji kwenye leseni za uchimbaji, uzalishaji madini, ajira pamoja na makusanyo ya maduhuli ya Serikali.

Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana  amezitaja Faida za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini kuwa ni wachimbaji wa madini kupata bei nzuri ya madini kutokana na uwazi uliopo sokoni.

Faida nyingie amezitaja kuwa ni wachimbaji wa madini kutokuwa na haja ya kutorosha madini, kitendo ambacho kilikuwa ni hatari kwani kilikuwa kinasababisha wachimbaji kupokonywa madini yao na serikali pamoja na kukabiliwa na kifungo pindi wanapobainika kutenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa Afisa Madini Mkazi huyo,faida nyingine ni Serikali  kupata takwimu sahihi za mauzo ya mazini na urahisi wa kukusanya mapato yaliyokuwa yakipotea kutokana na utoroshaji wa madini.

“Kuongezeka kwa tija ya utendaji kazi kwenye ofisi za madini kutokana na watumishi wa ofisi hizo kufanya shughuli nyingine badala ya kupoteza muda mwingi kuwafuatilia wachimbaji wa madini migodini,Serikali kupata takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo ya madini nchini na Kuongezeka kwa mapato ya serikali yatokanayo na shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ni faida nyingine za uwepo wa masoko haya’’,alisisitiza Nkana.


Hata hivyo Katika kutatua changamoto wanazokabiliana nazo wachimbaji wadogo wa Madini mkoani Ruvuma, Serikali inajenga kituo cha Umahiri kwa ajili ya  wachimbaji wadogo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amezitaja faida za kituo hicho kuwa ni uwepo wa takwimu za wachimbaji wadogo katika mkoa wa Ruvuma,upatikanaji wa maeneo  yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo na utoaji wa mafunzo na maarifa  kwa Wachimbaji wadogo kupitia wadau mbalimbali.

 Faida nyingine za kituo hicho amezitaja kuwa ni kuwepo kwa Mfumo wa kutathmini mashapo ya madini yaliyopo ili kufanya uchimbaji wenye tija,Mikopo na mitaji kwa wachimbaji wadogo,uongezaji wa thamani madini na masoko na utatuzi wa migogoro ya uchimbaji madini inayojitokeza.