Trump kushiriki kwenye mkutano wa kuisaidia Lebanon

Watu zaidi ya 60 bado hawajaonekana tangu kutokea mlipuko mkubwa nchini Lebanon siku nne zilizopita. Mlipuko huo uliotokea kwenye bandari ya mji mkuu Beirut na umesababisha vifo vya watu zaidi ya 150.

Waziri wa afya wa Lebanon amesema watu wengine 120 miongoni mwa watu 5000 waliojeruhiwa wamo katika hali mbaya sana.

Wakati huo huo rais Donald Trump amesema atashiriki kwenye mkutano wa kimataifa juu ya kuisaidia Lebanon utakaoandaliwa na Ufaransa.

Trump amesema baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwamba wote wanataka kuisaidia Lebanon. Trump aliyasema hayo katika ujumbe mfupi kwa njia ya Twitter.