Wakazi wa Kisabi wamlilia Waziri Lukuvi



Na Omary Mngindo, Ruvu.

WAKAZI wa Kitongoji cha Kisabi Kata ya Mtongani Kibaha vijijini Mkoa wa Pwani, wanamuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, awasaidie waondokane na manyanyaso wanayoyapata.

Wakazi hao wametoa kilio hicho wakizungumza na Waandishi wa Habari Kitongojini hapo, ambapo walisema wanaishi eneo hilo kwa hofu kubwa, wakitishiwa watabomolewa nyumba zao wakidaiwa hapo ni mali ya Taasisi ya DIMALA iliyokuwa inajihusisha na ufugaji.

Wakijitambulisha kwa majina ya Fatima Ramadhani, Hassani Nzolelanga, Kassimu Bakari, Asia Ngoengo na Hamisi Abdallah, Asia alisema kuwa mwaka 2014 walikuwa wanaishi ng'ambo ya mto Ruvu, wakakumbwa na mafuriko wakaamua kuingia eneo hilo na kuweka makazi.

"Baada ya mafuriko, tuliona hapa kuna msitu mkubwa, tukasafisha tukaishi, kutokana na msitu mkubwa paliitwa machinjioni, waharifu walifanya mauwaji na ubakaji, pia hata Mwenyekiti wetu wa Kitongoji tulimchagua tukiwa hapahapa, tunashangaa leo tunaambiwa tumevamia" alisema Asia.

Zolelanga alisema kuwa baada ya wao kufika hapo mpaka sasa wanajishughulisha na kilimo cha nsinu sanjali na bustani, ambazo kipato chao wanakitumia kuendesha shughuli za kifamilia ikiwemo kusomesha watoto na nyingine nyingi.

"Tumeishi kwa miaka sita, serikali yeru inatutambua, lakini tunasikitishwa na kauli kutoka kwa viongozi wetu kutuambia tunatakiwa tuondoke, wakidai ni eneo la DIMALA, tunahoji mbona haliendelezwi badala yake kulikuwa na msitu mkubwa?," alihoji Zolelanga. 

Bakari alieleza kuwa pamoja na kuelezwa kwamba eneo hilo ni mali ya Taasisi hiyo, lakini ndani yake vimepimwa viwanja vinauzwa kati ya shilingi laki tatu mpaka milioni moja, huku wakitakiwa na wao wakavinunue na kwamba wasitegemee kuishi hapo.

Abdallah aligusia mchakato wa kufungua tawi la Chama Cha Mapinduzi, ambapo wameshakamilisha taratibu zote, lakini walipofika viongozi wa chama ngazi ya Kitongoji walikataa kuwafungulia, wakidai hapo sio sehemu yao, wakati tayari wameshakabidhi fedha kwa ajili ya kupatiwa kadi.

"Tumekamilisha taratibu zote za kufunguliwa kwa tawi, lakini mwisho wa siku viongozi wetu wamesema kuwa eneo hilo tunatakiwa kuondoka, tubomoe nyumba zetu tuliache wazi kwani ni mali ya DIMALA, cha kishangaza humohumo viwanja vimekatwa watu wanauziwa," alisema Abdallah.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Yussufu Mzee alisema kuwa amewazuia kujenga nyumba za kudumu kutokana na eneo hilo kuwa la Kampuni ya DIMALA, iliyokuwa inajihusha na ufugaji wa ng'ombe, huku akiongeza kuwa aliwaambia wajiorodheshe ili afikishe ombi kwa Meneja kama wataweza kuwapatia eneo.

"Walileta orodha yao ya watu watu si zaidi ya 45, wakati wao wapo zaidi ya 100 nikawaambia warudi wawaandike na wenzao wote, ili itakapowafikia walengwa kama watawapatia wajue wapo wangapi na ukubwa gani wa ardhi ambayo wataitoa, lakini mpaka sasa sijawaona ndio wanakuja na Waandishi wa Habari," alisema Mzee.