DC Komba awaeleza mazito wahitimu wa mafunzo ya awali ya JKT.

 


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Vijana waliohitimu mafunzo ya awali ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) kwamujibu wa sheria kupitia operesheni UCHUMI WA KATI 2020 katika Kikosi cha Jeshi namba 843( 843KJ) kilichopo wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi wameaswa wawapime wagombea wa nafasi za uongozi katika maeneo matatu.


Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba katika hafla ya kufunga mafunzo ya awali ya vijana waliojiunga na JKT kwa mujibu wa sheria katika Kikosi cha Jeshi namba 843 kilichopo wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi.


Komba ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema vijana hao wamehitimu mafunzo hayo kipindi ambacho nchi ipo katika uchaguzi mkuu wa kuchagua wagombea wa nafasi ya urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar, wà bunge ,wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani. Kwahiyo wao watumie nafasi hiyo kuwapigia kura waombaji wenye sifa muhimu kwa kuwapima katika maeneo matatu makuu.


Komba aliyataja maeneo hayo ambayo ni vigezo vya msingi kwa muombaji anayefaa kuchaguliwa kuwa ni ahadi wanazotoa zinalenge kuimarisha umoja, amani na utulivu. Kwani baadhi ya wagombea  wanashindwa kuwaeleza wananchi ni kwajinsi gani wataendeleza umoja, amani na utulivu uliopo nchini. Kwahiyo wagombea wa aina hiyo hawafai na hawasitahili kunyimwa kura.


" Nukta ya pili muhimu ni kuangalia maneno yanayosemwa  na ahadi zinazotolewa yanalenga kulifanya taifa mizizi yake ijikite kwenye uchumi wa kati au zinalenga kutumia vibaya raslimali tulizonazo na kuturudisha nyuma kutoka kwenye hatua kubwa tuliyofikia? Wagombea wenye nia yakuturudisha nyuma mkawakatae,"  Komba alitaja eneo la pili kwa msisitizo.


Mkuu wa wilaya huyo wa wilaya ambae ni miongoni kwa wakuu wa wilaya wapya na vijana alitaja eneo la tatu ambalo wahitimu hao wanatakiwa kuwa makini kuwasikiliza na kuwapima wagombea ni iwapo wagombea hao kauli zao zinalenga kulifanya taifa kujitegemea na kuwa huru katika kufanya maamuzi bila ya kuingiliwa na  watu na mataifa mengine au litegemee misaada na maamuzi ya watu wa nje na kuuza utu na thamani yetu kama taifa.


Aidha Komba aliwaasa wahitimu hao watumie mafunzo hayo wiki saba kwa tija. Ambayo tija ya mafunzo hayo yataanza kuonekana wakiwa vyuoni kwa kusaidia taifa kwa kadri watakavyoweza kwa kutumia mafunzo hayo.


Alisema licha ya mafunzo hayo kufanyika kwa muda mfupi lakini imetosha kuonekana kwamba Jeshi la Kujenga Taifa ni kisima cha kuelea vijana kuwa wazalendo, wakakamavu, raia wema wenye moyo wa kujitolea na kujitegemea. Mambo ambayo ni muhimu kwa ujenzi wa uchumi, ulinzi wa taifa na maendeleo ya nchi.


Komba aliwakumbusha wahitimu hao kwamba lengo la kuanzishwa Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwaandaa vijana wawe raia wema ambao wamejazwa moyo wa uzalendo, kujitegemea na kujitolea, kujituma na utayari wa kulitumikia taifa. Sifa ambazo vijana hao wanazo baada ya kupata mafunzo hayo.

Post a Comment

0 Comments