Watatu kizimbani Kisutu kwa uhujumu uchumi


 Watu watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwemo kosa la uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha Dola za Marekani zaidi ya laki tatu mali ya Kampuni ya SMCI ya Marekani.

Washitakiwa hao Deogratius Masika, William Kimonge wakazi wa Dar es salaam na Youssoufa Sabo raia wa Cameroon wamesomewa shitaka lao  mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi Cassian Matembele.

Inadaiwa kati ya Decemba 2016 na Januari 2017 jijini Dsm, waliilaghai Kampuni ya SMCI ya Marekani nakujipatia dola za Marekani  laki tatu na ishirini wakidanganya kuwa wataisambazia Kampuni hiyo tani elfu tano za korosho kutoka Mtwara wakati sio kweli.

Katika shitaka la tatu na la nne ambalo ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,  washitakiwa hao wanadaiwa kuilaghai Kampuni ya SMCI ya nchini Marekani nakujipatia Dola elfu kumi na tano za Marekani wakidanganya kuwa wataisambazia Kampuni hiyo tani elfu kumi za Korosho kutoka Mtwara kwenda Dsm wakati sio kweli.

Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la kuilaghai Kampuni hiyo na kujipatia Dola za Marekani zaidi ya  laki tatu na kuzingiza kwenye Account ya CRDB yenye jina la JAW distributors limited, kwa lengo la kubadilisha kuwa fedha za Kitanzania.

Hata hivyo washitakiwa hao wamekana shitaka linalowakabili huku Hakimu anayeendesha shauri hilo kudai dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa namba mbili ambaye ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini Bondi ya milioni sitini na tisa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septamba 29 mwaka huu na washitakiwa wote wamerudishwa rumande.

Post a Comment

0 Comments