Afghanistan imedai leo kwamba imemuua kiongozi muhimu wa kundi la al-Qaeda aliye kwenye orodha ya watu wanaotafutwa zaidi na shirika la ujasusi la Marekani FBI.
Inatajwa kuwa Husam Abd al-Rauf aliuliwa wakati wa operesheni iliyofanywa na vikosi vya Afghanistan mashariki mwa nchi hiyo, hali inayoashiria uwepo wa wanamgambo hao nchini humo katika wakati wanajeshi wa Marekani wakiwa wanajitayarisha kuondoka nchini Afghanistan licha ya kuendelea kwa umwagaji damu.
Mauaji ya al-Rauf, anaejulikana pia kama Abu Muhsin al-Masri yametokea baada ya wiki kadhaa za mapigano, ikiwa ni pamoja na shambulio la bomu lililotokea jana kwenye kituo kimoja cha elimu karibu na mji mkuu Kabul na kusababisha vifo vya watu 24.
Kundi linalojiita Dola la Kiislam IS limedai kuhusika na shambulio hilo. Wakati hayo yakijiri, serikali ya Afghanistan inaendelea kupambana na wanamgambo wa Taliban huku pande hizo mbili zikiwa zinafanya mazungumzo ya amani nchini Qatar.
