Oct 17, 2020

Serikali ya sisitiza vyama vya Michezo kuzingatia Utawala Bora

  Muungwana Blog 2       Oct 17, 2020

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amevitaka Vyama vya Michezo nchini kuzingatia suala la utawala bora katika kusimamia na kuendesha michezo.

Mheshimiwa Mwakyembe ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa kujadili Mafanikio ya Sekta ya Michezo yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano nchini kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta hiyo kwa lengo la kukuza uchumi.

”Katika Kipindi cha Miaka Mitano  kuanzia 2015 – 2020 nimefarijika kusikia takribani wanamichezo 2018 wamepata mikataba ya ajira kupitia michezo ya kulipwa na takribani wanamichezo 54 wamepata ajira nje ya nchi,” Dkt.Mwakyembe.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Michezo alivipongeza vyama vyote vya michezo kwa mafanikio  waliyojipatia katika kipindi cha miaka mitano ikiwemo kushiriki mshindano mbalimbali katika ngazi za kimataifa na kujipatia ushindi.

”Katika kipindi cha miaka mitano nimefarijika kuona jitihada za viongozi mbalimbali wa vyama vya michezo katika kukuza michezo na kama mtendaji wa wizara yenye dhamana napenda kuwaahidi kuwa serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika kufanikisha sekta ya michezo inazidi kukua na kutoa ajira kwa vijana,” alisema Dkt. Abbasi.


Aidha, Mwenyekiti  wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Bw. Leodgar Tenga alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake katika kuendeleza michezo huku akieleza kuwa viongozi wa vyama vya michezo nchini  wanaikumbuka kauli yake ya kuwa sisi ni taifa kubwa la watu milioni 60 na hutuwezi tukawa tunashindwa kupata ushindi katika mashindano mbalimbali duniani, ambapo alisisitiza kuwa kauli hiyo imekuwa ikiwahamasisha kuongeza juhudi zaidi kila siku.

”Napenda kumshukuru Mheshimiwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwani amekuwa akitupatia mchango wa kifedha mara nyingi na kwenye michezo mbalimbali kila tulipokuwa tukikwama kushiriki mashindano  ya nje ya nchi na pia tunampongeza kwa kulinda amani ya taifa letu kwani michezo haiwezi kukua katika taifa lisilokuwa na amani,” alisema Bw. Tenga.

Halikadhalika  Mwenyekiti huyo wa Baraza alitoa ombi kwa serikali kwa niaba ya wanamichezo la kujenga kwa  Bwawa la Kuogelea (International Swimming Pool) lenye vigezo vya Kimataifa ili mchezo huo uweze kupata sehemu rasmi ya kufanyia mazoezi pamoja ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Ndani (Indoor Stadium) nchini kwa lengo la kufanikisha mashindano mbalimbali ya michezo.

Pamoja na hayo naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Bw.Wallace Karia alitoa alieleza kuwa katika sekta ya mpira wa miguu katika kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kupata mataji tisa katika mashindano mbalimbali na kuishukuru serikali kwa kuwa nao bega kwa bega katika kufanikisha mashindano mbalimbali.

Mkutano huo wa kujadili mafanikio ya sekta ya michezo kwa miaka mitano yaliandaliwa na Baraza la Michezo Tanzania  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliyotoa udhamini wao ikiwemo Azam Media Group,Serena Hotel na wengine na katika mkutano huo mgeni rasmi Mhe.Waziri alikabidhiwa  Mkakati wa kufanya vizuri katika Michezo  kwa miaka mitano na Mwenyekiti wa BMT.

 

logoblog

Thanks for reading Serikali ya sisitiza vyama vya Michezo kuzingatia Utawala Bora

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment