Ethiopia imesema imewaua wapiganaji 550 wa Tigray


Shirika la utangazaji la Ethiopia limesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wamewaua wapiganaji 550 wa Tigray (TPLF) wakati huu ambapo mzozo katika eneo hilo la Kaskazini ukishika kasi.

Madai hayo hayajathibitishwa na mashuhuda huru.

Hii imekuja wakati ripoti zikionesha kutokea kwa vifo vya mamia ya watu kwa pande zote mbili.

Siku ya Jumanne, mkuu wa wapiganaji wa TPLF, Debretsion Gebremichael aliishutumu serikali ya nchi jirani ya Eritrea kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya jimbo la Tigray.

Shutuma hizo zilikanwa na pande zote, serikali ya Eritrea na Jeshi la taifa la Ethiopia.

Msemaji wa kamati ya dharura ya serikali, Redwan Hussein, siku ya Jumanne alisema kuwa bado kuna uwezekano wa mazungumzo kati ya serikali na mamlaka za Tigray.

Lakini alisema “vifaa vilivyokamatwa na vikosi vilivyokamatwa na vikosi vilivyo vitiifu kwa TPLF lazima viharibiwe, watu wanaoshikiliwa na vikosi vya Tigray waachiliwe na wale walioanzisha mashambulizi wafikishwe mbele ya mikono ya sheria”.

Wakati huo huo polisi wa Ethiopia wamesema kuwa wanajeshi 17 - wakiwemo maafisa wakuu - wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya njama wakati jeshi la kaskazini lilipodaiwa kushambuliwa wiki iliyopita wamekamatwa.

Maafisa wamesema kuwa waliharibu mawasiliano kati ya uongozi na jeshi lote la taifa.

Haijulikani kama watuhumiwa hao walijibu shutuma hizo.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia