MKAAZI wa Bandamaji Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, amepandishwa katika mahakama ya Mkoa Mahonda kosa la kupatikana na dawa za kulevya.
Kijana huyo ni Issa Silima Sheha (27) alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Rashida Said.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya, jambo ambalo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 11 (a) sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za Zanzibar.
Alidai kwamba, mshitakiwa huyo alipatikana na kete 42 zinazosadikiwa ni dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa gramu 1.386 jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mshitakiwa alidaiwa kufanya kosa hilo Disemba 25, 2018 majira ya saa 5:20 usiku, katika kijiji cha Kiwengwa Mafarasi Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alikataa kosa na kuomba kupewa dhamana, ombi ambalo halikukubaliwa kwa upande wa mashitaka kutokana na kiwango cha dawa alizokamatwa nazo kijana huyo.
Wakili Rashida alidai kuwa kwa kupitia kifungu cha 151 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar, hairuhusu kupewa dhamana mshitakiwa kutokana na kiwango kikubwa alichokamatwa nacho.
Hata hivyo upande huyo wa mashitaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba tarehe nyengine sambamba na wito kwa mashahidi.
Mahakama ilikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 23 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
