Maafisa wanasema majadiliano ya kutafuta maelewano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza yataendelea hadi wiki ijayo huku mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya Novemba 19 ukiwa fursa ya mwisho ya kupata mwafaka.
Msemaji wa Umoja wa Ulaya Daniel Ferrie ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa wanajizatiti ili maelewano yapatikane na kwamba kutakuwa na mazungumzo mjini London mwishoni mwa wiki hii na wiki ijayo yatafanyika mjini Brussels.
Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya anayeyafuatilia mazungumzo hayo kwa karibu amesema hakuna kilichobadilika, na isitoshe Uingereza imebadilisha msimamo wake katika masuala kadhaa iliyokuwa imefikia maelewano na Umoja wa Ulaya.
Muda wa maelewano hayo kupatikana ni mfupi mno kwa kuwa ni sharti mabunge ya Uingereza na Umoja wa Ulaya yaidhinishe mkataba huo kabla Januari mosi ambao ndio muda wa mwisho wa kipindi cha mpito cha baada ya Brexit.
0 Comments