Rais Donald Trump anataka kura za Wisconsin zihesabiwe tena ambako mpinzani wake Joe Biden anatabiriwa kushinda kwa kura 20,000.
Saa kadhaa kabla ya siku ya mwisho ya kuwasilisha malalamishi Jumatano kufika, timu ya kampeni ya Trump inataka kura za kaunti ya Milwaukee na Dane zihesabiwe tena.
Bwana Trump amekuwa akidai kwamba kulikuwa na wizi wa kura na kukataa kumkabidhi mwenzake rasmi madaraka.
Bwana Biden amesema hatua ya kuchelewa kukabidhi madaraka itaathiri zaidi kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Timu ya kampeni ya Trump imewasilisha kesi kadhaa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu ingawa maafisa wa uchaguzi wanasema hakuna ushahidi wowote unaoonesha uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu.
Hata hivyo, licha ya ukosefu wa ushahidi, karibu nusu ya wapiga kura wa Republican wanaamini madai ya rais ya wizi wa kura ni ya kweli, kulingana na kura ya maoni ya shirika la habari la Reuters
Rais mteule Joe Biden wa chama cha Democrat inakadiriwa kuwa alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya kura milioni 5.6.
Upande wa kura za wajumbe zenye kuamua nani ndiyo anayeibuka na ushindi, Joe Biden amepata kura 306 huku Donald Trump akipata kura 232.
