Idadi ya waliopoteza maisha yao kufuatia machafuko ya kampeni nchini Uganda imefikia watu 30. Hii ni kwa mujibu wa taarifa za polisi nchini humo.
Akizungumzia machafuko hayo kwa mara ya kwanza, rais Yoweri Museveni ameonya kuwa wale waliohusika katika kuchochea ghasia hizo watakiona cha mtema kuni na anawalaumu wageni kwa kufadhili machafuko hayo.
Kwa upande wao, wanaharakati wa haki za binadamu wanaikosoa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kwa kushindwa kudhibiti vyombo vya usalama ambavyo inadaiwa vimewaua watu wasio na hatia ambao hawakuwa miongoni mwa waandamanaji.
Huku taarifa za ghasia za kampeni zikiendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku ya tatu mfululizo, polisi imearifu kuwa idadi ya waliopoteza maisha yao imefikia watu 30 na wengine wengi miongoni mwa zaidi ya sitini waliopata majeraha wamo katika hali mahututi.
Miongoni mwao ni waandishi habari watatu. Kulingana na taarifa hizo watu 48 wana majeraha ya risasi. Wanaharakati wa haki za binadamu wameshtumu vyombo vya usalama kwa mauaji hayo. Sarah Birete mkurugenzi wa Kituo cha utawala wa kikatiba CCG ni mmojawapo wa wanaharakati aliyekemea machafuko hayo.
