Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas ametaka wasanii wasifungiwe ovyoovyo nyimbo na filamu zao bila kushirikishwa.
Badala yake, ameagiza wawe wanaitwa kwa hatua ya kuelezwa kosa lao kwa lengo la kuwasaidia badala ya kuwaadhibu.
Dk Abbas ameyasema hayo leo Jumatano Desemba 2, 2020 alipokutana na wasanii wa filamu na sanaa za maonyesho, katika kikao kazi baina yao na Serikali kilichohudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk Kiagho Kilonzo.
Katibu mkuu huyo ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, amesema ofisi yake isingependa kuona wasanii wakifungiwa kazi zao bila kuelimishwa kwa nini wanafungiwa.
“Wasanii ni watu wakubwa, wasichukuliwe poa ikiwemo kuwafungia ovyo kazi zao bila kuwataarifu. Unakuta watu wametumia gharama kubwa kutengeneza wimbo au filamu halafu anaamka asubuhi anasikia kuna kiongozi ameita waandishi wa habari anautangazia umma eti anafungia kazi fulani, hii haikubaliki,” amesema Dk Abbas.
Katika kulifanya jambo hilo vizuri zaidi, Dk Abbas amesema endapo kuna makosa yamebainika, ni vema msanii akaitwa na kuelezwa kasoro na utaratibu wa kufuata kusudi arekebishe kazi yake, ama aianze upya.
“Muite muweke chini, mpatie hata chai chapati na juisi, kisha fanya naye mazungumzo taratibu kwa kumuelewesha kosa lake, mwisho wa siku mnaweza kuipangia kazi daraja ya kutazamwa na muda gani, au kama anaweza kurekebisha afanye hivyo,” amesema Dk Abbas.
Akizungumzia kikao hicho, Dk Abbas kimelenga kupata maoni kutoka kwa wasanii hao ya kuangalia namna gani ya kukuza sekta ya filamu nchini iweze kusonga mbele.
Kwa upande wao wasanii wamesema kuna haja kubwa ya wao kusikilizwa badala ya utaratibu unaotumika sasa wa kufungia kazi zao bila kushirikishwa wala kupatiwa taarifa.
Sanday Temba, amesema lakini pia kuna haja kwa wasanii kupatiwa elimu ya mara kwa mara ikiwamo ya namna ya kuishi ki-staa, kujieleza mbele za watu na kujua nini wanapaswa kujibu na kutojibu kwa umma.
0 Comments