Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis amemtaka mkandarasi mshauri wa mradi wa ujenzi wa Soko la kisasa la mjini kati kuwepo eneo la mradi kwa saa 24 ili kuharakisha ujenzi huo.
Ameyasema hayo Januari 9 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya mkakati wa soko kuu na stendi ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza, ambapo amesisitiza wasimamizi kuwepo kazini usiku na mchana na kuhakikisha majengo yanayojengwa yanakuwa na ubora.
Pia Naibu Waziri amemtaka msimamizi mshauri wa kampuni ya OGM Consultancy, kuhakikisha katika miradi hiyo miwili kunakuwa na usimamizi wa muda wote ili kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.
Naye Mbunge wa jimbo la Nyamagana, Stansilaus Mabula amesema kiu ya Wananchi wa Mwanza ni kuona miradi hiyo miwili inakamilika kwa wakati.
“Tutaisimamia miradi hii kwa umakini ili iwe na tija kwa wananchi, kwani mji wetu una wafanyabiashara wengi na kwa sasa wanafanyabiashara katika mazingira yasiyo na ubora.
"Nashukuru Wizara ya Fedha kutoa fedha kutekeleza miradi hii ya kimkakati, lakini kulingana na kukua kwa mji huu naomba miradi mingine inapo buniwa wizara iwe tayari kutoa fedha kwa wakati ili kuharakisha ukuaji wa mji na kusaida maendeleo kwa uharaka," alisema Mabula.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sima Costantine na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk Philis Nyimbi wamekiri kupokea agizo la Naibu Waziri huyo na kuhakikisha watashirikiana kurahisisha upatikanaji wa saruji.
Naye Mhandisi wa Halmshauri ya Jiji la Mwanza, Tunaye Mahege alisema ujenzi wa soko unaogharimu Sh20.7 bilioni umefikia asilimia 8 ya ujenzi na stendi ya Nyegezi inayogharimu iSh15.8 bilioni umefikia asilimia 10 na miradi yote miwili inatarajiwa kukamilika April 2022.
