Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis atakutana na mhubiri maarufu wa madhehebu ya Kishia Ayatollah Ali Sistani wakati wa ziara yake ya kwanza kabisa nchini Iraq inayopangwa mwezi Machi.
Kadinali Louis Sako, wa Kanisa Katoliki la Wakaldea nchini Iraq amesema itakuwa "ziara ya kibinafsi" kati ya viongozi hao wawili wa kidini katika makaazi ya Sistani kwenye mji wa Najaf, bila kuwepo matukio yoyote ya wazi.
Sistani mwenye umri wa miaka 90, hajawahi kuonekana hadharani na ni nadra sana kuwapokea wageni. Uthibitisho wa mkutano huo unafanyika wiki chache baada ya sehemu nyingine za ziara hiyo ya Papa kupangwa.
Sako amesema anatumai viongozi hao wawili watasaini waraka kuhusu "udugu wa kibinaadamu kwa amani ya ulimwengu'', ambao ni rasimu ya dini mbalimbali inayolaani vitendo vya itikadi kali. Papa Francis alisaini waraka huo na mhubiri maarufu wa Kisunni Sheikh Ahmed al-Tayeb, imamu mkuu wa Al-Azhar, Februari 2019.
