Wakati kila baada ya sekunde mbili, msichana mwenye umri chini ya miaka 18 anaolewa duniani na kufanya idadi ya wanaoolewa kufikia 12 milioni kwa mwaka, kwa Tanzania Mkoa wa Shinyanga unatajwa kuongoza kwa ndoa za wasichana chini ya umri wa miaka 18.
Takwimu hizo zilitolewa juzi na taasisi isiyo ya kiserikali ya Msichana Initiative Organization, huku ikielezwa kuwa wasichana wawili kati ya watano wanaolewa chini ya umri stahiki nchini.
Akizungumza wakati wa kuwatangaza ‘machampion’ (bingwa) 10 wa kusaidia mapambano ya kutokomeza ndoa za utotoni, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Rebeca Gyumi, alisema hali hiyo inasababishwa na kuwapo kwa sheria kandamizi ikiwamo sheria ya ndoa ya 1971 katika vifungu 13 na 17.
Gyumi alisema tatizo la wasichana kuolewa chini ya umri unaofaa lipo karibu mikoa yote, lakini akataja baadhi ya mikoa ambayo kuna kiwango cha juu ambayo ni Shinyanga wenye asilimia 59, Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48) na Mbeya iliyofikisha wastani wa asilimia 45.
“Tunalenga kuwajenga watoto wa kike na kufanya mabadiliko chanya katika jamii, ndio maana tumeteua ‘machampioni’ wenye uzoefu na mwanga katika masuala haya ili kuwepo na utendaji mzuri katika mapambano,”alisema Gyumi. Waliochaguliwa kuwa machampioni ni pamoja na wabunge akiwamo Ndaisaba George (Ngara- CCM) Margaret Sitta (Urambo-CCM), Ng’wasi Kaman (Viti Maalum-CCM), Aida Khenan (Nkasi Kaskazini-Chadema) na Neema Lugangira (Viti Maalum-CCM).
Wengine ni mwenyekiti wa Mtando wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, Valerie Msoka, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (Juwakita) Shamim Khan na mkurugenzi wa JengaHub na Championi wa haki za watoto, Nancy Sumari.
Wengine ni mwanaharakati wa masuala ya wasichana, Devotha Tweva na mkurugenzi wa shirika la Agape Shinyanga John Myole
Alisema wamewapitisha watu hao wakitegemea kuona sauti zikipazwa kila mahali kuhusu kulinda ustawi wa jamii, kwa kuhakikisha wasichana wanalindwa na hatimaye kuepukana na ndoa za utotoni.
Mkurugenzi huyo alisema wanafanya kazi hiyo ili kuwafanya wasichana wajiamini, kujitambua na kufahamu haki zao, sambamba na kuchochea mabadiliko ya sheria na sera zinazomkandamiza na kumnyima haki mtoto wa kike.
Kwa upande wake, John Myola alisema muungano wa nguvu moja utachochea mabadiliko yanayoweza kuwafanya wasichana kuwa na maono chanya na kufanya mageuzi nchini. Alisema kwa sasa kuna mabadiliko ya ndoa hizo tofauti na zamani.
