TAKUKURU Manyara inamsaka Mganga wa Kienyeji alieruka dhamana

 


Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoani Manyara inamtafuta Mganga wa Jadi aitwaye Luhanga Mindi Mabeshi baada ya kuruka dhamana.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru Manyara Holle Makungu imeeleza kuwa Mabeshi alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara iliyokaa chini ya 

Mheshimiwa Simon Kobello kwenda jela miaka miwili  katika kesi namba CC.05/2019 ilitolewa tarehe 09/09/2020 bila ya mshtakiwa kuwepo mahakamani kwa kuwa aliruka dhamana.

Makungu amesema Mabeshi kabla ya kukamatwa na kushtakiwa, alikuwa akijitambulisha kuwa ni mpelelezi kutoka Umoja wa Waganga wa Jadi na Tiba Asili Tanzania (UWAWATA). 

Hivyo alikuwa amejipa kazi ya kuwakagua waganga wa jadi kisha kuwaomba rushwa kwa maelezo kuwa wanafanya tiba chonganishi hadi alipokamatwa na kushtakiwa Mahakamani kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki mbili (Sh. 200,000/=).

Hati za kumkamata zimeshatolewa na Mahakama, hivyo yoyote atakayemuona atoe taarifa TAKUKURU iliyokaribu au namba zetu za dharura 113. Mabeshi huwa anapendelea kutembelea Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida na Manyara.

Post a Comment

0 Comments