Shirika la Afya Duniani, WHO tawi la Ulaya limesema leo kuwa ni mapema mno kulegeza vizuizi vya kukabiliana na janga la corona barani Ulaya licha ya kupungua kwa visa vipya katika nchi nyingi. Hans Kluge, mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya amesema 30 kati ya nchi 53 za Ulaya zimeshuhudia kupungua pakubwa kwa visa hivyo katika kipindi cha siku 14.
Kluge hata hivyo amesema viwango vya maambukizi kote Ulaya bado vipo juu mno, na kuathiri mifumo ya afya na utoaji huduma na kufanya iwe mapema mno kulegeza vizuizi.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehorfer amesema nchi hiyo inajiandaa kuweka marufuku dhidi ya watu wanaoingia nchini kutokea Uingereza, Ureno, Brazil na Afrika Kusini ili kupunguza usambaaji wa aina mpya ya virusi vya corona vinavyoambukiza kwa kasi ambavyo vimeripotiwa katika nchi hizo.
Seehorfer ameapa kuwa Ujerumani itaendelea na mipango yake hata kama Umoja wa Ulaya hautakubaliana na na hatua za aina hiyo.
