WHO yasema haina mpango wa kubadilisha muongozo wake kuhusu barakoa za vitambaa


Shirika la afya duniani limesema WHO limesema halina mipango ya kubadilisha muongozo wake wa kupendekeza barakoa za vitambaa huku aina mpya ya virusi vya corona vikienea

Ujerumani na Austria zimefanya uvaaji wa barakoa za kitabibu kuwa lazima katika uchukuzi wa umma na madukani na kuruhusu tu aina maalumu ya barakao za FFP2 mbali na zile za vitambaa huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hatari zinazotokana na kusambaa kwa haraka kwa aina hiyo mpya ya virusi.

Maria Van Kerkhove, kiongozi wa kiufundi wa shirika la WHO kuhusiana na virusi vya corona, amesema kuwa aina hiyo mpya ya virusihuenda ikawa na ''ongezeko zaidi la maambukizi'' lakini kutokana na utafiti wa aina hiyo mpya ya virusi vilivyogunduliwa nchini Uingereza na Afrika Kusini, hakuna dalili ya kubadilika kwa njia ya maambukizi na kwamba virusi hivyo bado vinasambazwa kama awali.

Shirika la WHO linashauri kwamba barakoa za vitambaa zisizokuwa za kitabibu zinaweza kutumiwa na umma kwa ujumla chini ya umri wa miaka 60 na ambao hawana matatizo mengine ya kiafya.

Wakati huo huo shirika la WHO linapendekeza barakoa za kitabibu kutumika kwa wafanyikazi wa afya katika mazingira ya kliniki, mtu anayeugua, anayesubiri matokeo ya uchunguzi wa Covid-19 ama aliyethibitishwa kuwa na maambukizi na watu wanaomshughulikia mtu aliyethibitishwa kupata maambukizi.

Pia zinapendekezwa kwa watu wa umri wa miaka 60 ama zaidi ama walio na matatizo mengine ya kiafya kutokana na hatari ya kupata maambukizi zaidi. Van Kerkhove amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa shirika hilo halipangi kubadilisha msimamo wake na kwamba mataifa yana uhuru wa kujifanyia maamuzi.

Kerkhove amesema kuwa wataendelea kuangalia ushahidi ambao wameuona lakini kutokana na takwimu zilizoonekana kutoka mataifa yaliona na aina hiyo mpya ya virusi, hakuna mabadiliko katika njia za maambukizi.

Hata hivyo amesema kuwa iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote, watabadilisha na kutoa muongozo mwengine vilivyo.

Van Kekhove pia amesema kuwa barakoa sio tu njia ya pekee ya kupunguza kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona na kwamba hakuna sulushisho moja pekee linaloweza kudhibiti janga hilo.

Post a Comment

0 Comments