Miamba ya soka nchini Hispania, vilabu vya Barcelona na Real Madrid vyote kwa wakati mmoja vimeandamwa vilio kutokana na wachezaji wake wengi wa vikosi vya kwanza kuwa na majeraha yanayopelekea wawili hao kushindwa kufanya vizuri.
Kocha wa Barcelona, Ronald Koeman amesema wachezaji wake watatu wamepata majeraha hii leo hivyo wataukosa mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya kombe la Copa del rey utakaochezwa kesho Februari 10, 2021 dhidi ya klabu ya Sevilla.
Wachezaji watakaokosekana ni, mshambuliaji Martin Braithwaite, kiungo Miralem Pjanic na mlinzi wa kulia Sergino Dest wenye maumivu ya misuli na nafasi zao zitachukuliwa na Ilaix Moriba, Alex Collado na Konrad de la Fuente kutoka timu ya vijana ya klabu hiyo ‘Lamasia’.
Baada ya nyota hao watatu kupata majeraha, orodha ya wachezaji wa Barcelona wenye majeraha kwa sasa imeongezeka na kufika 8 wakiwemo Ronald Araujo, Sergio Roberto, mkongwe Gerard Pique, Philippe Coutinho na Ansu Fati.
Kwa upande mwingine,
Wapinzani wa Barcelona, klabu ya Real Madrid huenda ikacheza mchezo wa usiku wa leo wa La Liga dhidi ya Getafe bila ya nyota wake 8, 7 wakisumbuliwa na majeraha wakati Toni Kroos akitumikia adhabu ya kuoneshwa kadi tatu za manjano.
Wachezaji ambao watakosekana kutokana na majeraha ni nahodha wake, Mkongwe Sergio Ramos aliyefanyiwa upasuaji wa goti hapo jana , Alvaro Ordiozola, Federico Valverde, Eden Hazard, Rodrygo, Isco na mlinzi wake mkongwe Marcelo.
Wachezaji ambao huenda wakarejea dimbani usiku wa leo baada ya kuonekana kupona majeraha yao ni pamoja na mlinzi wa kulia Daniel Carvajal na mlinzi wa kati, Eder Militao.
