Na John Walter-Babati
Kituo cha Msaidie mlemavu awaze kujitegemea (MMA) kilichopo chini ya kanisa katoliki parokia ya Galapo wilayani Babati Mkoani Manyara kimetoa msaada wa mabati kumi kwa familia ya Bi. Anastazia Aribogasti ambaye ametelekezewa watoto wawili ambao wana ulemavu wa viungo.
Hata hivyo tayari mama huyo ameshaanza kujenga msingi wa nyumba yake pamoja na kufyetua matofali.
Akizungumza wakati wanapotoa msaada huo katibu wa shirikisho la watu wenye ulemavu mkoa wa Manyara Peter Sanka amesema walimfuatilia baba huyo ambaye ameitelekeza famalia hiyo na kuondoka na watoto wengine ambao hawana ulemavu kwa ajili ya kuendelea kuitunza familia bila mafanikio.
Aidha Katibu huyo ameiomba jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuiwezesha familia hiyo kwa kuwa jamii ndiyo walezi pekee wa familia hiyo kwasasa.
Kwa upande wake padri wa Parokia ya Galapo George Kamula amewaomba watu kuwa na utamaduni wa kuwasaidia watu ambao wanapitia kwenye mazingira magumu kwani kwa kufanya hivyo ndiyo namna ya kuwapa faraja na kuwaonyesha upendo kwa vitendo.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Hala Theofili John amewataka wananchi kushikamana na kwa pamoja ili kuweza kuwasaidia watu wenye uhitaji na kuachana na dhana ya kutegemea misaada kutoka nje pekee kwani kila mtu anaweza kufanya hivyo.
Bi.Anastazia Aribogasti mara baada ya kupatiwa msaada huo amewashukuru wishukuru serikali na wadau waliofanikisha kumsaidia kupata msaada huo wa mabati kumi.
