Oscar Waluye, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Orkitikiti iliyopo kijiji cha Engong'ongare wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara amefikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za udanganyifu wa mtihani.
Wakati akifikishwa mahakamani, mamlaka yake ya nidhamu imemfukuza kazi.
Kwa mujibu taarifa ya kaimu mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Alli Sadiki Hajji mwalimu huyo amefunguliwa kesi namba 31/2021 leo Februari 3, 2021.
Hajji amesema Waluye ameshtakiwa kwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba iliyofanyika Oktoba 2020 kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 23 na 24 (1) sheria ya baraza la mitihani la Taifa.
Amesema kesi hiyo ya jinai imefikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Joakim Mwakyolo na mwendesha mashtaka wa polisi, Wilfred John.
Amebainisha kuwa mtuhumiwa amekana mashtaka hayo na alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, kupelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Februari 16, 2021.
