Televisheni ya taifa ya Myanmar imeonya leo kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji wanaovunja sheria, huku makundi makubwa yakiandamana kupinga mapinduzi ya kijeshi.
Maelfu ya watu waliingia mitaani mwishoni mwa wiki kushinikiza kuachiwa kwa kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi na kuirejesha madarakani serikali iliyochaguliwa na raia.
Jeshi lililompindua Suu Kyi wiki moja iliyopita, mpaka sasa limejizuwia kutumia nguvu kubwa kuzima maandamano, lakini polisi ilitumia maji ya kuwasha kuwatawanya waaandamanaji.
Taarifa iliyosomwa na mtangazaji wa kituo cha serikali cha MRTV, ilisema kumekuwepo na ukiukaji wa sheria na vitisho vya kutumia nguvu na makundi yanayotumia kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu