Maelfu ya wakulima wanaoandamana nchini India leo walizifunga kwa saa tatu barabara kuu nchini humo kuongeza shinikizo kwa serikali ibadili sheria mpya za kilimo wanazodai zinayapendelea makampuni makubwa.
Njia kuu zilifungwa kwenye maeneo kadhaa ya majimbo ya Haryana na Punjab huku maandamano yalifanyika pia kwenye jimbo la Jammu Kashmir, Bangalore na Pune.
Kiongozi wa muungano wa wakulima amesema kuzifunga barabara ni kitendo cha ishara na wamekitumia kufikisha ujumbe kwa serikali pamoja na kuwatanabaisha raia wengine sababu za wao kufanya maandamano.
Picha zilizorushwa na vituo vya televisheni kutoka mji wa Kurukshetra zimeonesha wakulima wanaondamana wakiwapatia chakula maderava wa malori na magari waliokwama kutokana na vizuizi walivyoviweka.
Wakulima wanadai kuwa sheria hizo mpya zitawafanya kuwa masikini zaidi lakini serikali kwa upande wake imesema zinanuwia kukifanya kilimo cha India kuwa cha kisasa.
