Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo ameukosoa vikali uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC ambao unafungua njia ya kufanyika uchunguzi wa uhalifu wa kivita uliofanywa kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.
Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Netenyahu ameutaja uamuzi huo wa ICC kuwa ubaguzi dhidi ya wayahudi na ameapa kutumia kila njia kupambana na kile alichokitaja "ukandamizaji wa haki usio wa kawaida" Jana Ijumaa, mahakama ya ICC ilipitisha uamuzi kwamba ina mamlaka ya kisheria kuhusu yanayotendeka ndani ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ikiwemo ukingo wa magharibi, Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki.
Uamuzi huo utamwezesha mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda kuanzisha uchunguzi kubaini iwapo makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binadamu umetendwa kwenye maeneo hayo.
