Washindwa kuhudhuria masomo kisa Sh200 za kivuko

 


Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kagera na Mgumile katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma Tanzania, wameshindwa kuhudhuria masomo kwa wakati baada ya kukosa fedha kiasi cha Sh200 za kuvuka kivuko cha Mto Luiche.


Mto huo unaelezwa kuwa na wanyama wakali wakiwamo mamba na viboko hali inayohatarisha usalama wao.


Wakizungumza leo Jumanne Februari 9, 2021 wamesema wanaiomba Serikali iwajengee daraja litakalowawezesha kuvuka salama wakati wa kwenda na kurejea shuleni.


Mwanafunzi wa shule ya Kagera, Benjamin Salum amesema mara nyingi wamekuwa wakirudishwa nyumbani na kukataliwa kuvuka kwenda shule kama hawana kiasi hicho cha fedha.


“Mara nyingi wanaturudisha nyumbani kwa sababu ya kukosa fedha za kivuko ambazo nyumbani hatupewi, kama tukifanikiwa kuvuka wakati wa asubuhi kwenda shule basi wakati wa kurudi inakuwa shida tunakaa hadi usiku tukiwa tumechoka na njaa zinatuuma," amesema Salum.


Mwanafunzi wa shule ya Mgumile, Mariam Musa amesema wanaenda shuleni kwa shida na kwa wiki wanaingia darasani mara tatu kutokana na wazazi wao kukosa fedha za kulipia kivuko hicho.


Diwani wa Kagera, Gregory Ebelezo amesema kata yake yenye mitaa minne ina wakazi 9,040 wanaotumia kivuko hicho kwa shughuli zao za kila siku.


"Wanafunzi wamekuwa wakipata shida hasa nyakati za kwenda na kurudi shule, lakini tulishazungumza na uongozi wa eneo hilo na kukubaliana kutowatoza fedha ya aina yoyote wanafunzi hao, wapite bure kuwahi masomo na wakati wa kurudi nyumbani,"amesema Ebelezo.


Meneja wa Wakala wa barabara za vijijini na mijini (Tarura), Mkoa wa Kigoma, Issa Liyanga amesema kivuko hicho kipo kwenye mpango wa serikali.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi