Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO tawi la Ulaya limeonya leo kuwa janga la virusi vya corona limeathiri vibaya matibabu ya saratani, huku huduma za saratani zikivurugika katika theluthi moja ya nchi za kanda hiyo.
Akizungumza leo katika Sika ya Kimataifa ya kupambana na Saratani, Mkurugenzi Mtendaji wa WHO barani Ulaya Hans Kluge ameonya kuwa athari ya janga la corona kwa ugonjwa wa saratani barani Ulaya ni janga kubwa.
Miongoni mwa mataifa 53 wanachama wa WHO barani Ulaya, ambayo ni pamoja na nchi kadhaa za Asia ya Kati, moja kati ya nchi tatu imeshuhudia kuvurugwa kwa sehemu au kikamilifu huduma za saratani kwa sababu ya shinikizo linalotokana na ugonjwa wa Covid-19 kwa mifumo ya afya na vizuizi vya usafiri.
Kluge amesema baadhi ya nchi zinashuhudia uhaba wa dawa za saratani zikiwemo nchi zenye utajiri wa raslimali.
