Polisi wa Uganda wanasema wamemkamata mtu anayedaiwa kuwa msafirishaji wa watoto aliyepigwa picha katika uchunguzi wa BBC wa mwaka 2011 kuhusu kafara ya binadamu.
Mshukiwa huyo, dereva wa lori, alichukuliwa katika mji wa mpakani wa Elegu kaskazini mwa Uganda mwishoni mwa wiki.
Msemaji wa polisi Fred Enanga alithibitisha kuwa atahamishiwa kwa Kurugenzi Maalum ya Upelelezi ya polisi katika mji mkuu Kampala.
Anasema polisi walijua tukio hilo baada ya video ya mtuhumiwa iliyochukuliwa miaka 10 iliyopita hivi karibuni kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo anadai kuongoza mtandao wa wafanyabiashara wa watoto nchini Uganda ambao huwateka watoto kwa ajili ya shughuli za kishirikina aina nyingine za unyonyaji.
Katika ripoti hiyo, mtuhumiwa huyo alijisifu jinsi alivyowapata watoto hao kwa timu ya BBC, wakijifanya kama wanunuzi wanaopanga kusafirisha watoto kwenda Uingereza.
Bwana Enanga anasema polisi watapitia madai yaliyomo katika ripoti hiyo na kwamba hakuna mashtaka yoyote ambayo yametolewa dhidi yake bado.
Mapema mwezi Mei bunge lilipitisha Muswada wa Kuzuia na Kukataza Dhabihu ya binadamu ambao, ikiwa utasainiwa kuwa sheria, kuna uwezekano wa kuwepo kwa adhabu ya kifo kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kutekeleza au kufadhili kafara ya wanadamu.
