Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF, Henrietta Fore, amelihimiza kundi la nchi tajiri zaidi duniani G7 kuchangia dozi milioni 150 kwa nchi ambazo hazina chanjo.
Shirika la UNICEF limesema leo kwamba nchi za kundi la G7 pamoja na Umoja wa Ulaya, zina uwezo wa kutoa asilimia 20 tu ya dozi zao bila ya kudhuru malengo yao ya kampeni za utoaji chanjo.
Hayo ni kulingana na utafiti ambao umefanywa na shirika la Airfinity la Uingereza.Uingereza inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi za G7 zikiwamo Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Italia na Marekani kwenye mkutano wa kilele mwezi Juni.
Shirika la UNICEF limesema kufikia wakati wa mkutano huo, mpango wa kimataifa wa ugavi wa chanjo, COVAX, utakuwa na upungufu wa dozi milioni 190.
Upungufu huo umesababishwa kwa sehemu na maambukizo mabaya ambayo yameikumba India ambayo ilipaswa kutengeneza chanjo nyingi kwa mpango wa COVAX lakini sasa imelazimika kuzitumia dozi hizo.
